Mabomu ya mapipa yawauwa watu 15 katika mji wa Aleppo

Uharibifu wa mabomu Aleppo Haki miliki ya picha AFP
Image caption Matumizi ya mabomu ya mapipa, yanayosababisha hasara kubwa, yamekuwa yakitumiwa sana katika mzozo wa Syria

Wanaharakati nchini Syria wanasema kuwa watu 15 wameuawa katika mashambulio ya mabomu ya anga yaliyorushwa kwenye wilaya inayodhibitiwa na waasi ya Aleppo.

Afisa wa Uangalizi wa masuala ya haki za binadamu nchini Syria mwenye makao yake nchini Uingereza amesema kuwa ndege za utawala wa Syria zilirusha vilipuzi viwili vilivyosheheni makombora yaliyotengenezwa ndani ya mapipa kwa dakika kadhaa tofauti ambayo yaliangukia karibu na hema ambako jamaa wa watu waliouawa kwa mabomu wiki iliyopita walipokuwa wakipokea rambi mbali.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema bomu la kwanza liliuvutia umati wa watu kukimbilia eneo la tukio, ambako bomu jingine lilipiga na kuwauwa watu zaidi na kuharibu gari la kubebea wagonjwa.

Inaaminiwa kuwa makumi kadhaa ya watu wamejeruhiwa na idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.

Mazungumzo ya hivi karibuni baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi kuhusu kuanzishwa upya kwa muda wa usitishaji mapigano kote nchini Syria yalimalizika bila mafanikio.