Rio 2016: Mwanariadha wa zamani Kenya Kipchoge Keino ahojiwa

Kipchoge Keino
Image caption Kipchoge Keino asema: ``Acha kila mtu aubebe msalaba wake. Kila atakaye patikana na hatia lazima akabiliane na sheria.''

Mwanariadha maarufu wa zamani wa Kenya Kepchoge Keino anahojiwa kwa uchunguzi na polisi wa Kenya kufuatia usimamizi mbovu wa timu ya Kenya iliyoshiriki michezo ya mjini Rio de Janeiro.

Akiwa mwenye machungu, Keino ameiambia BBC kwa njia ya simu kwamba polisi wanamuuliza ni kwa nini alishindwa kuongoza ipasavyo kama mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya Olyimpiki ya Kenya (NOCK) iliyovunjiliwa mbali na waziri wa michezo Hassan Wario.

Lakini Keino anahisi Wario alikuwa na pupa kwa kuharakisha kuiadhibu ``badala ya kuitakasa kwanza ofisi yake.''

Keino alisema kuwa hajafanya kosa lolote, na alituma ujumbe mkali kwa viongozi wenzake wa Nock kwamba :``Acha kila mtu aubebe msalaba wake. Kila atakaye patikana na hatia lazima akabiliane na sheria . Sina hatia kwasababu sijaiba chochote''.