Mmoja wa makamanda wa IS auawa nchini Syria

Abu Muhammad al Adnani
Image caption Abu Muhammad al Adnani

Kundi la wapiganaji la Islamic state limetangaza kuwa mmoja wa kamanda wake mwandamizi ambae ni msemaji wa kundi hilo, Abu Muhammad al-Adnani ameuwawa nchini Syria.

Taarifa ya mtandao unaohusiana na kundi hilo Amaq, inasema kuwa Abu Muhammad ameuwawa wakati alipokuwa kwenye operesheni za kijeshi katika jimbo la Allepo.

Mtandao huo haukutoa taarifa nyengine zaidi.

Wanajeshi wa marekani wamethibitisha kuwa walikuwa wamemlenga Abu Muhammad al-Adnani lakini wanasema bado walikuwa wakichunguza matokeo ya shambulizi la anga la siku ya Jumanne katika mji wa Al-Bab, kaskazini mashariki ya jimbo la Allepo.

Marekani inamuelezea Abu Muhammad al-Adnani kuwa ni mpangaji mkuu wa mashambulizi ya nje ya I-S na imesema kuwa kifo chake kinaweza kuwa nukta muhimu ya kushindwa kwa kundi hilo.