Samsung yasitisha uuzaji wa Note 7 sababu ya betri

Samsung Note 7 Haki miliki ya picha AFP

Kampuni ya kuunda simu ya Samsung imesema itasitisha uuzaji wa simu maarufu ya Galaxy Note 7 kutokana na matatizo ya betri.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kutokea ripoti Marekani na Korea Kusini kwamba simu hizo zilikuwa "zinalipuka" wakati au baada ya kuwekwa chaji.

Hilo limejiri wiki moja tu kabla ya mshindani wake mkuu Apple kuzindua simu mpya zaidi ya iPhone.

Jumatano, kampuni ya Samsung ilisema imesitisha usafirishaji wa simu hizo kwa kampuni tatu kuu zinazosafirisha simu hizo hadi maeneo mbalimbali duniani ili kufanya uchunguzi zaidi.

Mtu mmoja katika YouTube, anayesema anaishi Marekani, aliweka mtandaoni video inayoonesha Galaxy Note 7 ikiwa imeungua na skrini yake kuharibika.

Ariel Gonzalez, kwenye video hiyo aliyoweka 29 Agosti, anasema simu yake ilishika moto baada yake kuitoa kutoka kwenye chaja rasmi ya Samsung, chini ya wiki mbili.

Picha zaidi za Galaxy Note 7 zilizoungua ziliwekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Kakao Story, maarufu nchini Korea, mnamo 30 Agosti.

Haki miliki ya picha Ariel Gonzalez
Image caption Simu ya Galaxy Note 7 inadaiwa kuungua baada ya kutolewa kwenye chaja