Mbunge ataka watu wenye jinsia 2 kutambulika Kenya

Mbunge wa Kenya Issack Mwaura
Image caption Mbunge wa Kenya Issack Mwaura

Mbunge mmoja nchini Kenya amelitaka bunge la taifa hilo kupitisha sheria inayotambua jinsia nyengine ya tatu ili kumaliza ubaguzi dhidi ya wale wanaotumbulika kuwa na jinsia mbili.

Issac Mwaura pia anataka ufadhili wa upasuaji wa kubadili jinsia pamoja na hamasa ili kukabiliana na unyanyapaa miongoni mwa watu wenye jinsia mbili.

''Wananiona mimi kama mtu mwenye laana '',mtu mmoja aliyezaliwa mwanamke na ambaye baadaye alianza kuwa na tabia za kiume aliambia BBC.

Watu wenye jinsia mbili hawatambuliki moja kwa moja kuwa wanaume ama wanawake.

James Karanja, ambaye anatambulika kuwa mwanamume alisema kuwa alipozaliwa alikuwa na jinsia zenye utata na wazazi wake walimtambua kimakosa kuwa msichana.

''Jina langu rasmi ni Waithera,jina nililopatiwa na mamangu baada ya jinsia yangu kutambulika kimakosa nilipozaliwa''.

''Walidhani mimi ni msichana na kumbe ni mvulana.Ninatoka kutoka familia ya umasikini kwa hivyo hawakupata fursa ya kunipeleka hospitali kubaini jinsia yangu''.

Bwana Karanja kwa sasa anafanyiwa upasuaji ,ili kubadilisha jinsia yake na anasema kuwa matibabu hayo ni ya gharama ya juu sana.