Rais Robert Mugabe atoa mzaha kuhusu afya yake

Robert Mugabe Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Mugabe amesema alikuwa Dubai kwa masuala ya kifamilia

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amepuuzilia mbali taarifa za hivi karibu za uvumi juu ya afya yake, kwa kutoa mzaha kwamba alikufa na akafufuka.

Akionekana mwenye furaha, Mugabe mwenye umri wa 92, aliyasema hayo alipokuwa akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Harare akitokea nje ya nchi.

Taarifa ya safari yake ilisema kuwa ndege yake ilikuwa ikielekea mashariki mwa Asia, na kwamba badala yake ilikwenda Dubai.

Bw Mugabe alisema kuwa alikwenda huko kwa masuala ya kifamilia.

Mnamo mwezi Mei, Mke wa Mugabe, Grace, alisema kuwa mumewe ataongoza nchi hata akiwa kaburini.

Taarifa za uvumi kuhusu safari zake za ndege na nyinginezo, zilisababisha kuenea kwa tetesi kwamba afya ya Bw Mugabe ilikuwa mbaya na kwamba alikwenda Dubai kwa matibabu ama hata alikuwa tayari amepoteza maisha.

Tovuti ya Gazeti linalochapishwa kila siku la Southern Daily, ilituma makala yenye kichwa cha habari "Robert Mugabe anauwa kiharusi, Mnangagwa sasa ndie rais wa mpito wa Zimbabwe".

Emmerson Mnangagwa ni makamu rais wa Zimbabwe.