Muhtasari: Habari kuu leo Jumatatu

Miongoni mwa habari kuu leo, John Kerry atashauriana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kuhusu vita Syria na maelfu wameandamana kupinga rais mpya Brazil.

1. Chama cha Angela Merkel chashindwa jimboni Ujerumani

Haki miliki ya picha Getty Images

Chama tawala cha Ujerumani chake Chancela Angela Merkel, CDU kimepata pigo kubwa baada ya kushindwa katika jimbo anakotoka Merkel la Mecklenburg-( Pomerania Magharibi).

CDU kilipata nafasi ya tatu kwenye kura hiyo ya majimbo ambayo ilighubikwa na suala la wakimbizi. Wapiga kura wamekosoa vikali sera ya Bi Merkel ya uhamiaji, na chama kinachopiga wahamiaji kuingia Ujerumani AFD kinatarajiwa kuchukua nafasi ya pili.

2. Muda wa kuhebu kura Hong Kong waongezwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Nathan Law aliongoza maandamano ya wanafunzi 2014

Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea eneo la Hong Kong katika uchaguzi wa bunge.

Wapiga kura wengi walijitokeza na imewalazimu maafisa wa uchaguzi kuomba kuongezewa muda zaidi wa kuhesabu kura hizo.

3. G20: Xi Jinping ataka mikakati ya ustawi

Haki miliki ya picha Getty Images

Viongozi wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani wanaendelea na kongamano ambapo limeingia siku ya pili nchini China.

Rais wa China Xi Jinping amewaomba viongozi hao kuweka mikakati ya kusaidia ukuaji wa uchumi na ustawi.

Aidha ametaka juhudi zaidi kuhakikisha utandawazi unaafikiwa na maeneo yote ya dunia.

4. Kerry kushauriana na Lavrov kuhusu vita Syria

Haki miliki ya picha AFP

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema anashauriana zaidi na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov pembezoni mwa mkutano wa G20. Mazungumzo hayo yatajadili jinsi ya kumaliza mapigano nchini Syria, ikiwemo kuweka njia salama za kupeleka misaada ya dharura.

5. Maelfu waandamana kumpinga rais Brazil

Haki miliki ya picha AP

Polisi katika mji wa Sao Paulo, Brazil wametumia vitoa machozi kuyatawanya maandamano makubwa zaidi ya kupinga Rais mpya, Michel Temer.

Maandamano zaidi dhidi ya kiongozi huyo yalifanyika katika mji wa Rio de Janeiro.

Waandamanji hao wengi kutoka chama cha Rais aliyeondolewa madarakani Dilma Rouseff wametaka kufanyika uchaguzi mpya.

6. Sokwe wapungua sana mashariki mwa DR Congo

Haki miliki ya picha Reuters

Aina pekee ya sokwe anayepatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anakabiliwa na tisho la kuangamizwa.

Idadi ya sokwe hao aina ya Grauer imepungua kwa asilimia 70 katika miongo miwili kutokana na uwindaji haramu nchini DRC.