Kiongozi wa Ufilipino Duterte asema hakukusudia kumshambulia Obama

Rodrigo Duterte Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Watu 2,400 wameuawa katika vita dhidi ya mihadarati tangu Rais Rodrigo Duterte aingie madarakani Juni

Kiongozi wa Ufilipino Rodrigo Duterte amesema anajutia kwamba amatamshi yake kumhusu kiongozi wa Marekani Barack Obama yamefasiriwa kama matusi.

Bw Duterte amesema hayo baada ya Bw Obama kufuta mkutano wake na kiongozi huyo kutokana na maneno ya lugha chafu yaliyoelekezwa kwake.

Kiongozi huyo wa Ufilipino alikuwa amemweleza Bw Obama kama "mwana wa kahaba" na kuongeza kwamba hatakubali kuulizwa maswali kuhusu ukiukwaji wa haki za kibinadamu nchini mwake.

Alisema Ufilipino haitawaliwi na mtu yeyote. Ufilipino ilikuwa koloni ya Marekani.

Hayo yalijiri kabla ya kufanyika kwa mkutano wa viongozi wa nchi za Kusini Mashariki mwa bara Asia, mjini Laos.

Lakini kupitia taarifa, Bw Duterte amesema anajutia matamshi hayo.

Amesema wanadiplomasia wa Ufilipino na Marekani wanatarajia kuondoa uhasama na tofauti zilizozuka baina ya nchi hizo mbili.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Barack Obama alionywa na Bw Duterte "kuonyesha heshima"

Tangu kuingia madarakani, Bw Duterte ameendelea kutumia maneno makali, na kutumia lugha chafu kuwarejelea Papa Francis, maafisa kadha wa Umoja wa Mataifa, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na balozi wa Marekani nchini Ufilipino.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii