Mfahamu rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, kiongozi aliyemtusi Obama

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Duterte ameweza kukabiliana na utata unaomzingira na kuibuka na ushindi wa kishindo

Rodrigo "Digong" Duterte ni kiongozi ambaye msimamo wake na matamshi yake huzua utata mara kwa mara. Amegonga vichwa vya habari tena baada ya kuonekana kumtusi Rais wa Marekani Barack Obama na kumuita "mwana wa kahaba".

Duterte aliweza kukabiliana na utata juu yake na kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Ufilipino wa mwezi Mei.

Baada ya kula kiapo cha urais, Juni 30 Bw Duterte, ambaye kipindi kirefu aliishi mjini Davao kusini mwa nchi tangu aliposhinda, ana mamlaka ya kuongoza taifa hilo kwa muhula mmoja wa miaka sita.

Rodrigo "Digong" Duterte alizaliwa mnamo mwaka 1945 katika familia iliyojikita katika siasa za ndani ya nchi.

Wakati mmoja baba yake alikuwa gavana wa jimbo, na familia hiyo ilikuwa na uhusiano na familia zenye ushawishi mkubwa za Duranos na Almendrases katika jimbo Cebu, ambako baba yake aliwahi kuwa meya.

Bw Duterte amesomea taaluma ya sheria na alipanda cheo hadi kuwa mwendesha mashtaka kabla ya kuteuliwa kuwa naibu meya wa Davao wakati wa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Ferdinand Marcos mwaka 1986.

Alikuwa meya mwaka 1988 na kushikilia wadhfa huo kwa kipindi cha miaka 10, kabla ya kushinda kiti cha ubunge katika Bunge la Congress halafu akarejea kwenye kiti cha umeya mwaka 2001.

Duterte ambaye utawala wake ni wa kipekee kwa kuwa kiongozi mwenye sera za Kijamaa na mwanamageuzi kwa pamoja, sera zake za uchumi zilikuwa si za kuaminika wakati wa kapeni.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption wafuasi wa Duterte wanasema sifa yake ya ukali ndio wafilipino wanayohitaji kukabiliana na ufisadi na uhalifu

Alijijengea umaarufu kwa kupiga vita baadhi ya matatizo makubwa yanayowakabili Wafilipino - uhalifu, makundi ya uasi, na ufisadi. Yote haya yalipungua kwa kiwango kikubwa wakati alipokuwa kiongozi wa Davao, na kufanya mji huo kuwa mmoja wa miji salama zaidi nchini Ufilipino.

Kuzua utata mkubwa

Aliahidi kubadili mfumo wa utawala wa taifa kutoka kwa mfumo wa bunge moja kuu yenye hadi kwenye mabunge ya majimbo, ili kugawana vyema mali ya taifa.

Msemaji wake alisema kutakuwa na "mageuzi makubwa yatakayofanyiwa katiba ya nchi".

Pia alikuwa ameahidi "kuwaua wahalifu 100,000" akiingia ikulu ya rais, akiongeza kuwa angepatia vikosi vya usalama uwezo wa "kupiga risasi na kuuwa" washukiwa wanaokwepa kukamatwa.

Tayari kufikia sasa, washukiwa 2,5000 wameuawa.

Ili kutekeleza baadhi ya mipango yake, atahitajika kuungwa mkono na kupata idhini kutoka kwa Bunge la Congress.

Kutusi watu

Amewahi kutangaza hadharani kwamba Ufilipino, ambayo imekuwa mshirika mkuu wa Marekani, haitategemea sana Washington.

Kijamii, yeye huunga mkono wapenzi wa jinsia moja lakini ni mhafidhina katika masuala mengi ya kijamii. Amegusia kupiga marufuku unywaji pombe maeneo ya wazi na kutoa amri ya kutotoka nje kwa vijana.

Amekuwa akiwatusi watu mashuhuri. Alimwita Papa Francis "mwana wa kahaba" (Ufilipino ni taifa lenye Wakatoliki wengi). Amewahi kumtusi pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kwa kumuita "mwendawazimu" na majuzi alimweleza balozi wa Marekani nchini Ufilipino kama "mpenzi wa jinsia moja ambaye ni mwana wa kahaba".

Alifanya mzaha na kusema kwamba alipokuwa meya angekuwa mtu wa kwanza kumbaka mmishenari kutoka Australia aliyeuawa wakati wa fujo gerezani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Duterte aliwahi kusema kwenye mdahalo wa televisheni kwamba anaweza kuwauwa wanawe kama watatumia mihadarati.

Msimamo wake mkali umemfanya abandikwe majina ya "mtoa adhabu " na "Duterte Harry".

Kuwaua wanawe

Alisema kwenye mdahalo wa televisheni kwamba anaweza kuwauwa wanawe kama watatumia mihadarati.

Yote hayo yamemuongezea sifa miongoni mwa wengi nchini Ufilipino kama mtu anayeweza kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha mambo muhimu yanatekelezwa .

Amekuwa akilinganishwa na mgombea wa urasi wa Marekani Donald Trump, lakini alikataa kufananishwa naye, akisema kwamba Trump "hakubali maoni ya wengine, lakini mimi sivyo".

Bw Duterte ameoa mara mbili, ana watoto wanne, na miongoni mwao binti yake Sara - alikuwa meya kwa muhula mmoja kabla ya kurejea tena kwa baba yake .

Kwa sasa hana mke, lakini anadai kuwa na marafiki kadhaa wa kike.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii