Basi latumiwa kufunza vijana kompyuta Nairobi

Basi
Image caption Basi hilo huhudumia wanafunzi 25 kwa wakati mmoja

Katika ulimwengu wa sasa, huwa ni kama hitaji la msingi kijana kuwa na ujuzi wa kutumia kompyuta.

Ni ujuzi unaohitajika katika maeneo mengi ya kazi na hata katika kutekeleza shughuli za kila siku.

Lakini kwa vijana wengi ambao hukosa nafasi ya kujiunga na shule au vyuo vinavyotoa mafunzo ya kompyuta, huwa vigumu sana kupokea ujuzi huu.

Image caption Vijana wanaofaidika ni kutoka mitaa mitano duni Nairobi

Wengi hulazimika kulipia vyuo maalumu kupata fursa hii ilhali kwa wengine, kutokana na kazi wanazozifanya kila siku, huwa vigumu kupata muda.

Lakini wakfu wa shirika la Craft Silicon Foundation, unaomilikiwa na kampuni ya kuuza programu za kompyuta, umeanzisha mradi unaowawezesha vijana kujifunza kutumia komputa ndani ya basi ambalo ni darasa.

"Mimi natoka Kibera, kwa sababu nimejaribu kutafuta pesa ili niweze kujilipia masomo ya kompyuta. Kazi ninayoifanya mapato ni ya chini sana sijapata pesa ambazo zinaweza kunisaidia ili niweze kulipia masomo hayo," anasema mmoja wa wanafunzi hao, Wesley Soi.

"Masomo haya yamenisaidia sana."

Basi hilo huhudumia vijana maskini katika mitaa ya Kawangware, Mukuru, Korogocho, Kibera na Mathare.

Image caption Priya Budhabhatti

"Nilikuwa na shida mwenyewe pale nilipokuwa nikisoma. Nilikuwa na shida ya usafiri ndio maana nikazindua basi hili ili niweze kuwasaidia wengine wasipitie kile nilichopitia nilipokuwa mwanafunzi," anasema Priya Budhabhatti, mwanzilishi wa mradi huo.

"Nimeanza mradi huu kwa sababu wengine hawana karo ya kujiunga na taasisi mbalimbali na ndio maana basi hili litawafikishia elimu hadi mlangoni mwao,'

Masomo hayo hutolewa bila malipo.

Wanaotaka kunufaika huwasilisha maombi kwa wakfu huo na wakikubalika, huhudhuria masomo saa mbili kila siku.wenye basi, huwa kuna walimu wawili ambao huwapa mafunzo mafunzo ya msingi kuhusu kompyuta na jinsi ya kutumia programi tekelezi kama vile Microsoft Word, Microsoft Excel na Microsoft Access.

Image caption Mwanafunzi anajifunza komputa

Kwa sababu za kiusalama, basi hilo hutumia sana afisi za machifu. Hata hivyo,hakuna mchango mwingine wowote wa serikali katika mradi huo.

Miongoni mwa changamoto ambazo watekelezaji wa mradi huo wanakumbana nazo ni hali duni ya barabara ambayo hutatiza usafiri kutoka mtaa mmoja hadi mwingine.

Wakati mwingine, joto pia huzidi ndani ya basi.

Image caption Wanafunzi wanasomo komputa

Basi hilo hutumia nguvu za umeme kutoka kwenye betri ya gari au umeme kutoka kwa majengo yaliyo karibu lakini kukiwa na jua hutumia kawi ya jua, yaani sola.

Wanafunzi wanaonufaika na mradi huo wanatumai ujuzi watakaoupata utawafaa maishani.

Mmoja wao, Ignitius Laligola, anasema anatarajia hilo litamsaidia kutafuta kazi.

"Kusema kwa kweli nimepata mafufaa mengi kupitia basi hili. Sikuwa najua Miscroft Word na Microsoft Excel. Sikujua kuandika kwa kutumia kompyuta lakini hizo zote kwa sasa naweza. Hata naweza kuandika barua," anasema Jemimah Achieng.