Muhtasari: Habari kuu leo Jumatano

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, Syria imedaiwa kutekeleza shambulio la gesi ya sumu Allepo, hakimu Corsica, Ufaransa akakataa kuondoa marufuku ya Burkini.

1. Syria yadaiwa kutekeleza shambulio la gesi

Haki miliki ya picha UGC

Waokoaji katika eneo linalodhibitiwa na waasi mjini Allepo nchini Syria, wanasema helikopta za serikali zimetekeleza shambulizi la mabomu kwa kutumia mapipa ya gesi ya Chlorine. Mwanaharakati mmoja ameiambia BBC kwamba mtu mmoja ameuwawa na wengine 120 wameathiriwa.

Umoja wa Mataifa unasema, Syria inashuhudia mwanzo mpya wa mapigano ya kinyama.

2. Seneta wa Mexico aandaa mswada kukabili Trump

Haki miliki ya picha Reuters

Seneta mmoja nchini Mexico anasema atawasilisha mswada bungeni, unaopendekeza marekebisho ya mikataba yote iliyotiwa saini baina ya Mexico na Marekani, iwapo Donald Trump atachaguliwa kuwa rais mwezi Novemba. Miongoni mwa mikataba hiyo, ni ule uliosainiwa mwaka wa 1848, ambapo Mexico iliikabidhi Marekani Jimbo la California pamoja na maeneo yake mengine.

3. Helikopta yadunguliwa na genge Mexico

Ndege aina ya Helikopta imetunguliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge moja la jimbo la Mexico Michoacan, ambapo rubani pamoja na maafisa watatu wameuwawa.

Gavana wa jimbo hilo anasema helikopta hiyo ilikuwa ikifanya oparesheni ya kuwakamata viongozi wa genge hilo.

4. Wabunge waitaka Uingereza kutouzia Saudi Arabia silaha

Haki miliki ya picha EPA

Rasimu ya ripoti mpya ya kamati ya bunge la Uingereza inasema kuwa London inafaa kusitisha uuzaji wa silaha nchini Saudi Arabia, wakati uchunguzi ukiendelea kuhusu vitendo vya Saudi Arabia katika vita vya kiraia vinavyoendelea nchini Yemen.

Majeshi ya Saudi yamehusishwa na mauaji ya raia, pamoja na shambulizi la hospitali ya shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka MSF mwezi uliopita. BBC imeona nakala inayosema kwamba, tuhuma za ukiukaji huo ni lazima zilihusisha silaha kutoka Uingereza.

5. Wanachama 13 wa al-Qaeda wauawa Yemen

Haki miliki ya picha EPA

Majeshi ya marekani yanasema kwamba yamewauwa wanachama 13 wa kundi la kigaidi la Al Qaeda katika mashambulizi ya angani nchini Yemen. Taarifa inasema kuwa mashambulizi matatu ya kupambana na ugaidi yalitekelezwa kati ya tarehe 24 mwezi agosti na tarahe 4 mwezi septemba katikati mwa Yemen.

6. UN yatishia kuichukulia hatua Korea Kaskazini

Haki miliki ya picha AFP/Getty

Baraza la uslama la umoja wa mataifa limeikashifu vikali Korea Kaskazini, baada ya kutekeleza jaribio la makombora siku ya jumatatu. Baraza hilo lilitishia kuichukulia Korea Kaskazini hatua zaidi, ikiwa itakataa kusitisha majaribio ya silaha za kinyuklia na makombora.

7. Hakimu akataa kuondoa marufuku ya Burkini

Haki miliki ya picha Reuters

Mahakama moja mjini Corsica Ufaransa imekataa kuondoa marufuku dhidi ya wanawake wanaovalia vazi maalum la kuogelea la wanawake wa Kiislamu, Burkini. Mahakama kuu zaidi ya utawala nchini Ufaransa iliamua kwamba marufuku hiyo ilikuwa inakiuka sheria. Hata hivyo hakimu mjini Corsica ameamua kwamba marufuku hiyo ni halali, kwani amani ya umma ilikuwa imevurugwa.