Trump asema Putin 'ni kiongozi bora kuliko rais wetu'

Trump / Clinton Haki miliki ya picha AP

Donald Trump amemlimbikizia sifa rais wa Urusi Vladimir Putin yeye na mpinzani wake Hillary Clinton walipokuwa wakipokea maswali kutoka kwa wanajeshi wastaafu.

Mgombea urais huyo wa chama cha Republican amesema kiongozi huyo wa Urusi "amekuwa kiongozi kwa kiwango kikubwa kumshinda rais wetu (Obama".

Amesema hayo siku ambayo mkuu wa idara ya ulinzi ya Marekani ameituhumu Urusi kwa kupanda mbegu za uhasama na misukosuko duniani.

Bi Clinton kwa upande wake, ametetea uwezo wake wa kufanya maamuzi ya busara huku akiendelea kushutumiwa kutokana na sakata ya barua pepe.

Bi Clinton anadaiwa kutumia anwani ya kibinafsi kutuma na kupokea barua pepe rasmi za serikali, jambo ambalo baadhi wanasema huenda lilihatarisha usalama wa taifa.

Wagombea hao wawili walitokea jukwaani wakiwa wanafuata kwa vipindi cha nusu saa kila mmoja katika kikao hicho kilichofanyika New York, Jumanne usiku.

Bw Trump aliulizwa maswali na mtangazaji wa NBC Matt Lauer kuhusu matamshi yake ya awali ambapo alinukuliwa akimsifu Bw Putin.

Alijibu: "Ninaweza kumpa 82% (kwa uongozi)."

"Nafikiri anaponisifu, nitazikubali pongezi hizo, kweli kabisa?" aliongeza mfanyabiashara huyo, akisema Bw Putin amelidhibiti vyema sana taifa lake.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hillary Clinton amesema hataongeza majeshi ya Marekani nchini Iraq

Bw Trump pia alibashiri kwamba akichaguliwa kuwa rais Novemba, "Nafikiri tutaelewana vyema naye".

Hii si mara ya kwanza kwa Bw Trump kumsifu kiongozi huyo wa Urusi.

Desemba, alisema ilikuwa ni "heshima kubwa" pale Bw Putin alipomweleza kama "mtu mwenye kipaji".

Majuzi, Bw Trump alishutumiwa alipohimiza Urusi kufukua zaidi na kupata barua pepe ambazo Bi Clinton alifuta kutoka kwenye sava, ambazo inaaminika zilipotea.

Baadaye alijitetea na kusema alikuwa anatania.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii