Boko Haram wapigana wenyewe kwa wenyewe Nigeria

Abubakar Shekau Haki miliki ya picha AFP
Image caption Abubakar Shekau alianza kuongoza Boko Haram 2009

Wapiganaji wa kundi la Kiislamu la Boko Haram nchini Nigeria wamepigana wenyewe kwa wenyewe kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, duru za kiusalama zimeambia BBC.

Maelezo kuhusu mapigano hayo yaliyotokea katika eneo la Monguno, jimbo la Borno karibu na Ziwa Chad bado ni finyu kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano ya simu za mkononi maeneo hayo.

Mapigano yametokea baada ya kundi linalojiita Islamic State (IS) kutangaza mwezi uliopita kwamba Abu Musab al-Barnawi ndiye kiongozi mpya wa Boko Haram, na kumuondoa Abubakar Shekau.

Lakini Bw Shekau, ambaye awali alikuwa ametangaza kujiunga na IS, alisema bado anaongoza kundi hilo.

Baadhi ya wachanganuzi wanasema mgawanyiko katika kundi hilo huenda ukawafaa wanajeshi wa Nigeria katika juhudi zao za kukabiliana na wanamgambo hao.

Kufikia sasa, jeshi la Nigeria halijatamka lolote kuhusiana na mapigano hayo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii