Obama alipokutana na Duterte, kiongozi aliyemtusi

Obama na Duterte Haki miliki ya picha EPA
Image caption Rais Obama na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte waangaliana

Rais wa Marekani Barack Obama na kiongozi wa Ufilipino Rodrigo Duterte wamekutana ana kwa ana siku moja baada ya kiongozi huyo wa Ufilipino kuonekana kumtusi Bw Obama.

Jumanne, Bw Obama alifutilia mbali mkutano uliokuwa umepangwa kati ya wawili hao baada ya Bw Duterte kumuita "mwana wa kahaba".

Walikutana kwa njia isiyo rasmi muda mfupi kabla ya dhifa ya jioni ya viongozi wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia nchini Laos.

Msemaji wa serikali ya Ufilipino alisema alikuwa na furaha sana kwamba mkutano huo ulifanyika.

Maafisa wa Marekani walisema ulikuwa "mkutano mfupi" kabla ya dhifa iliyoandaliwa viongozi katika eneo la "kuketi viongozi".

Bw Obama na Bw Duterte wanadaiwa kuingia kwenye ukumbi wa dhifa nyakati tofauti na hawakuzungumza au kukaribiana wakati wa hafla hiyo iliyodumu saa moja na dakika 20.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bw Duterte aliketi katikati mwa Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev na Rais wa Indonesia Joko Widodo

"Walikuwa wa mwisho kuondoka ukumbini. Siwezi kusema walikutana kwa muda gani," waziri wa mambo ya nje wa Ufilipino Perfecto Yasay, aliyesafiri na Bw Duterte, aliwaambia wanahabari baadaye.

"Nina furaha sana kwamba hili lilifanyika."

Afisa wa White House alisema wawili hao "walifahamiana" katika "kikao kifupi" kabla ya chakula cha jioni.

Bw Duterte, alionekana kuvuka mipaka katika kikao na wanahabari awali pale aliposema hangekubali ukosoaji wa Bw Obama kuhusu vita dhidi ya mihadarati iwapo hilo lingeibuka katika mkutano wao uliokuwa umepangwa.

"Lazima uwe na heshima. Si kurusha tu maswali na taarifa. Mwana wa kahaba, nitakutusi katika mkutano huo," Bw Duterte alisema, akionekana wazi kumrejelea Bw Obama.

Baadaye alisema alijutia matamshi hayo.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption (Kushoto hadi Kulia) Rais Obama, Mke wa Waziri Mkuu wa Vietnam, Waziri Mkuu wa Vietnam Nguyen Xuan Phuc, Waziri Mkuu wa Laos Thongloun Sisoulith, Mke wa Waziri Mkuu wa Laos, Waziri Mkuu wa Thailand Jenerali Prayut Chan-o-cha, Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Sen, Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev, Rais Duterte, Rais wa Indonesia Joko Widodo.

Watu 2,400 walioshukiwa kuhusika katika ulanguzi wa dawa za kulevya wameuawa tangu Duterte aingie madarakani mwezi Juni.

Ameshutumiwa na jamii ya kimataifa lakini anaonekana kupendwa na baadhi ya Wafilipino kwa hilo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii