Duru za Israeli zimesema Mahmoud Abbas alifanyia kazi KGB

Mahmoud Abbas Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Msemaji wa Abbas ameelezea madai hayo kama yasiyo na msingi yanayotolewa na Israeli kiholela

Duru za Israeli zimedai kuwa kiongozi wa wapalestina, Mahmoud Abbas huenda alikuwa akifanyia kazi huduma za upelelezi za siri za usovieti miaka ya 1980.

Watafiiti kutoka vhuo kikuu cha Hebrew mjini Jerusalem wanasema stakabadhi zilizopatikana katika makavazi ya chuo kikuu cha Cambridge zinaonyesha kwamba Bw Abbas alikuwa mjumbe wa KGB alipokuwa akiishi mjini Damascus.

Msemaji wa Abbas ameelezea madai hayo kama yasiyo na msingi yanayotolewa na Israeli kiholela.

Amesema kuwa madai hayo yamebuniwa kwa lengo la kuzuwia juhudi za hivi karibuni za serikali ya Urusi za kuanzisha upya mazungumzo ya amani baina ya waisraeli na wapalestina.

Mapema wiki hii kiongozi huyo wa Palestina alisema kuwa amekubali kukutana na Bw Netanyahu mjini Moscow siku ya Ijumaa, lakini maafisa wa Israeli waliomba mkutano huo uahirishwe hadi tahehe nyingine ambayo haikutajwa.

Wawili hao walisalimiana kwa mikono mwaka jana katika mkutano wa dunia wa mabadiliko ya hali ya hewa mjini Paris, lakini hawajawahi kushiriki mazungumzo ya maana tangu mwaka 2010.