Arsene Wenger: Sitaki Jack Wilshere ahame Arsenal

Jack Wilshere

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

Wilshere, amechezea Arsenal mechi zaidi ya 100

Arsene Wenger amesema matumaini yake ni kwamba kiungo wa kati Jack Wilshere, ambaye kwa sasa ametumwa Bournemouth kwa mkopo, atasalia Arsenal maisha yake ya uchezaji.

Wilshere, 24, ambaye huchezea timu ya taifa ya Uingereza, alienda Bournemouth kwa mkopo wa msimu mmoja.

Ni mmoja wa wachezaji waliokua kutoka chuo cha kustawisha wachezaji cha Arsenal na aliwachezea mechi yake ya kwanza 2008 akiwa na miaka 16.

Lakini alicheza mechi tatu pekee klabu hiyo msimu uliopita kutokana na majeraha.

"Yeye ni mchezaji stadi sana, hahitajiki kufanya jambo jingine kunionyesha uwezo wake," amesema Wenger.

"Binafsi, natumai atasalia hapa maisha yake yote ya uchezaji."

Wenger amesema walizungumza na mchezaji huyo.

Bournemouth watakutana na West Bromwich Albion Jumamosi na Wilshere anatarajiwa kucheza.