Clinton afuta ziara ya California baada ya kuugua kichomi

Bi Clinton akiwapungia mkono wanahabari baada ya kuondoka nyumbani kwa bintiye Jumapili Haki miliki ya picha AP
Image caption Bi Clinton akiwapungia mkono wanahabari baada ya kuondoka nyumbani kwa bintiye Jumapili

Mgombea urais wa chama cha Democratic nchini Marekani Hillary Clinton amefuta mkutano wake wa kampeni jimbo la California baada yake kuugua.

Bi Clinton amechukua hatua hiyo baada ya kugunduliwa kwamba anaugua ugonjwa wa kichomi ambao pia hujulikana kama nimonia.

Kichomi ni ugonjwa wa mapafu. Dalili zake huwa ni pamoja na kukohoa, homa, uchovu, baridi na kutatizika wakati wa kupumua.

Jumapili, alilazimika kuondoka mapema kutoka kwenye hafla ya kukumbuka waathiriwa wa shambulio la kigaidi la 9/11 jijini New York.

Hafla hiyo ilikuwa ya kuadhimisha miaka 15 tangu kutekelezwa kwa shambulio hilo lililosababisha vifo vya karibu watu 2,900.

Saa chache baadaye, madaktari wake walisema alikuwa amegunduliwa kuwa anaugua ugonjwa wa kichomi siku mbili awali na kwamba alipewa dawa na kushauriwa kupumzika.

Baada ya kuondoka kwenye hafla hiyo ya Jumapili, ambapo video zilionesha akisaidiwa kutembea, alipelekwa nyumbani kwa dadake hapo karibu.

Maafisa wake walisema alikuwa amezidiwa na joto mwilini.

Alitokea baadaye na kuwaambia wanahabari: "Najihisi vyema kabisa. Ni siku nzuri hapa New York."

Baada ya hapo alielekea nyumbani kwake Chappaqua, New York.

Daktari wake Lisa Bardack alisema mgombea huyo amekuwa akitatizwa na "kikohozi ambacho kinahusiana na mzio".

Bi Clinton alikuwa amepangiwa kuelekea California Jumatatu kwa ziara ya siku mbili, ambapo miongoni mwa mengine angehudhuria mikutano cha kuchangisha pesa na pia kutoa hotuba kuhusu uchumi.

Viongozi wa chama cha Republican tayari wameanza kuibua maswali kuhusu uwezo wake kiafya wa kuhudumu kama amiri jeshi mkuu.

Mpinzani wake mkuu Donald Trump aliwaambia wafuasi wake mwezi jana kwamba mgombea huyo "hana nguvu za kiakili na kimwili" kuhudumu kama rais na kuongoza vita dhidi ya wapiganaji wa Islamic State.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bw Trump pia alihudhuria maadhimisho hayo ya miaka 15 tangu shambulio la 9/11

Maafisa wa Bw Trump kwa sasa bado hawajazungumzia habari za Clinton kuugua kichomi.

Mwezi uliopita, Dkt Bardack alisema "yuko buheri wa afya na katika hali nzuri ya kuhudumu kama rais wa Marekani".

Alisema amepata nafuu kabisa kutoka kwa upasuaji aliofanyiwa shingoni mwaka 2012 kuondoa damu iliyokuwa imeganda kwenye mishipa.

Maafisa wa kampeni wa Bi Clinton wamewatuhumu wapinzani kwa "kuendeleza uvumi na habari za kupotosha kuhusu afya ya Clinton".

Bi Clinton ana umri wa miaka 68. Mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump ana miaka 70

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii