Wabakwa kwa kula nyama ya ng'ombe India

Wanawake hao walibakwa nyumbani kwao katika wilaya ya Mewat Haki miliki ya picha TAPAS MALLICK
Image caption Wanawake hao walibakwa nyumbani kwao katika wilaya ya Mewat

Mwanamke mmoja nchini India amesema kuwa yeye pamoja na binamuye wa umri wa miaka 14 walibakwa na genge la watu na jamaa wengine wawili wakauawa baada ya kalaumiwa kwa kuwa waislamu waliokula nyama ya ng'ombe.

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 20 aliiambia BBC kuwa, wanaume wanne walifanya uvamizi huo katika jimbo la Haryana Kaskazini wiki mbili zilizopita. Lakini yeye anakana kula nyama hiyo ya ngombe.

Alisema kuwa wanaume hao waliwaua kwa kuwapiga mjomba wake na shangazi nyumbani kwao katika eneo la Mewat.

Waumini wengi wa dini ya kihindu huwatambua ng'ombe kuwa watakatifu na kuchinjwa kwa wanyama hao kumepigwa marufu katika majimbo mengi likiwemo jimbo la Haryana.

Haki miliki ya picha TAPAS MALLICK
Image caption Kisa hicho kimezua ghadhabu katika jamii ya eneo hilo

Washukiwa hao wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa yanayohusu ubakaji na mauaji.

Wilaya yenye waislamu wengi wa Mewat iliyo umbali wa kilomita 100 kutoka mji mkuu wa Delhi, hivi majuzi iligonga vyombo vya habari baada ya afisa wa cheo cha juu, kuwaambia waandishi wa habari kuwa polisi wataanza kukagua chakula cha biryani kuhakikisha kuwa hakina nyama ya ng'ombe.

Ubakaji na uhalifu katika misingi ya kijinsia ni masuala yaliyoangaziwa zaidi nchini India miaka ya hivi karibuni, baada ya kisa ambapo mwanafunzi alibakwa na kuuawa na kundi la watu mwaka 2012 mjini Delhi.