Norilsk Nickel yakiri lawama mto kugeuka 'rangi ya damu' Urusi

Picha iliyopigwa 8 Septemba , 2016 Haki miliki ya picha AFP/Greenpeacw
Image caption Maafisa wa Norilsk Nickel wamesema hakuna hatari yoyote kwa binadamu au wanyama

Kampuni kubwa ya kuzalisha vyuma nchini Urusi Norilsk Nickel imekubali kwamba kiwanda chake kilichangia maji katika mto mmoja kubadilika na kuwa rangi nyekundu.

Kampuni hiyo ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa nikeli duniani imesema mvua kubwa iliyonyesha tarehe 5 Septemba ilisababisha maji taka kumwagika kutoka kwa bwawa la kiwanda cha Nadezhda.

Maji hayo yaliingia katika mto Daldykan.

Hata hivyo, kampuni hiyo inasema tukio hilo halikuhatarisha kwa vyoyote vile maisha ya watu au wanyama pori.

Kampuni hiyo ilikuwa imekataa katakata kwamba ilihusika baada ya picha za maji ya mto huo yakiwa na rangi nyekundu kuanza kusambazwa mtandaoni wiki iliyopita.

Mwanaharakati wa shirika la Greenpeace Russia anasema bado ni mapema kubaini iwapo kuna madhara.

"Huwezi ukapuuzilia mbali hilo," Alexei Kiselyov ameambia shirika la habari la AFP.

Amesema kampuni ya Norilsk Nickel inadhibiti watu wanaoingia au kutoka rasi yote ya Taymyr, ambapo tukio hilo lilitokea, jambo ambalo linatatiza uchunguzi kuhusu uchafuzi uliosababishwa na kiwanda hicho.

Maafisa wa wizara ya mazingira walikuwa wamedokeza wiki iliyopita kwamba uchafu wa kemikali huenda ulikuwa umevuja kutoka kwa mabomba ya kiwanda hicho na kusababisha maji ya mto huo kubadilika rangi.

Norilsk Nickel ilikanusha madai hayo na hata kupakia mtandaoni picha zilizodaiwa kuonesha maji hayo yakiwa na "rangi ya kawaida" mnamo tarehe 7 Septemba.

Makundi ya wakazi yameituhumu kampuni hiyo kwa kupuuza .

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii