Video ya mwanamke akijifungua kwenye maji yashangaza

Huwezi kusikiliza tena
Lynn anajifungua baada ya muda mfupi

Video ya mwanamke akijifungua mtoto akiwa kwenye maji imevuma sana mtandaoni baada yake kuonekana kujifungua kwa urahisi kuliko kawaida.

Wanawake wengi hutatizika sana wanapojifungua lakini kwa Audra Lynn inaonekana kuwa kama shughuli rahisi sana.

Video yake akijifungua katika eneo la Orange , California inashangaza kwa sababu mtoto anaonekana kutoka baada ya misuli yake kujikaza mara chache tu.

Video yake ambayo imepakiwa katika mitandao ya Instagram na Facebook, imetazamwa zaidi ya mara 16 milioni tangu ilipopakiwa Septemba 3.

Mkunga Lisa Marie Sanchez Oxenham ambaye alipiga video hiyo anasema lilikuwa "tukio la kushangaza".

Haki miliki ya picha Lisa Marie Sanchez Oxenham
Image caption Audra Lynn na mumewe Pete wakiwa na mtoto wao

"Kile huwezi ukaona kwenye video hiyo ni kwamba kichwa kilikuwa tayari kimetoka. Kwa hivyo, namwambia Audra asubiri misuli ijikaze tena, na hapo ndipo mtoto anachomoka.

"Furaha ya mama inagusa sana. Anaposema 'mtoto wangu mvulana', inawafanya watu kulia. Ni tukio linalogusa moyo sana."

Video hiyo imesambazwa zaidi ya mara 100,000 kwenye Facebook na watu 23,000 wamechangia maoni.

Lisa Marie anasema hajashangaa sana kwamba video hiyo imevuma sana.

"Ninaamini video hii imevuma sana kwa sababu ni tukio zuri, la upendo, la faraghani na mazingira yametulia," anasema.

"Ni jambo ambalo huwa hatulihusishi na kujifungua tena na watu hawawezi kutosheka."