Wanajeshi wa Niger wauawa katika vita na Boko Haram

Msemaji wa jeshi la Niger anasema kuwa wapiganaji 30 waliuawa na wawili kukamatwa. Haki miliki ya picha AFP
Image caption Msemaji wa jeshi la Niger anasema kuwa wapiganaji 30 waliuawa na wawili kukamatwa.

Takriban wanajeshi saba nchini Niger wameuawa katika kipindi cha juma moja lililopita kufuatia makabiliano kati yao na wapiganaji wa Boko Haram ,jeshi la taifa hilo limesema.

Wanajeshi wa Niger wakisaidiana na wenzao kutoka Chad walivamia kambi ya wapiganaji hao na kuwaua 30 na kuwakamata wawili ,msemaji wa jeshi amesema.

Mashambulizi hayo mawili yalifanyika kusini mashariki mwa jimbo la Diffa karibu na mpaka na Nigeria,taarifa ilisema.

Wanajeshi watano waliuawa katika uvamizi mwengine siku ya Jumatatu asubuhi na wengine wawili wakauawa baada ya gari lao la kupiga doria kukanyaga bomu la ardhini,taarifa hiyo imeongeza.

Mashambulio ya miaka saba yanayotekelezwa na kundi la Boko Haram yamesababisha vifo vya maelfu ya watu nchini Nigeria ,ambapo ndio ngome kuu ya wapiganaji hao,pamoja na maeneo jirani ya Niger,Chad na Cameroon.