Ndege za miraa zawasili Somalia

Mira yawasili nchini Somalia baada ya marufuku kuondolewa na serikali ya taifa hilo Haki miliki ya picha AP
Image caption Mira yawasili nchini Somalia baada ya marufuku kuondolewa na serikali ya taifa hilo

Ndege mbili zilizokuwa zimebeba miraa zimewasili katika mji mkuu wa Somalia ,Mogadishu kulingana na mwandishi wa BBC Ibrahim Aden.

Hatua hiyo inajiri baada ya Somalia kuondoa marufuku ya ndege za Kenya zinazobeba miraa iliowekwa wiki moja iliopita.

Haijulikani ni kwa nini marufuku hiyo iliwekwa ,lakini iliondolewa siku ya Jumanne jioni baada ya mazungumzo kati ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud.

Mazungumzo hayo yalifanyika wakati wa mkutano wa viongozi wa kieneo mjini Mogadishu.

Maelfu ya Wakenya ,ikiwemo wakulima na wafanyibiashara wamepata hasara ya mamilioni ya madola.

Miraa huliwa ikiwa bado haijakaa kwa muda mrefu na huongeza kasi ya mafikira katika ubongo wa mwanadamu.

Wakati wa biashara ya kawaida ,zaidi ya ndege 15 za miraa huwasili mjini Mogadishu kila siku kutoka Kenya.

Kulingana na mwanaharakati wa Somalia anayepinga miraa Abukar Awale,ndege hizo huingiza mabagi 12,000 ya miraa kila siku ambayo huwa na thamani ya dola 400,000.