Uganda kuwatuza medali wabunge wa zamani

Bunge la Uganda Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bunge la Uganda

Bunge la Uganda linatarajiwa kutumia shilingi milioni 600 za Uganda kununua medali za kuwatuza wabunge 1200 wa zamani katika kipindi cha mwaka 1962 hadi mwaka 2012 kulingana na kituo cha runinga cha NTV.

Mpango huo wa kuwaheshimu viongozi hao ulipendekezwa na rais Yoweri Museveni ili kuadhimisha miaka 50 kulingana na ripoti.

Uganda iliadhimisha miaka 50 ya uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 2012.

Kiongozi wa upinzani Kizza Besigye na mkewe Winnie Byanyima ni miongoni mwa viongozi watakaopewa medali kulingana na ripoti za gazeti la The Daily Monitor.

Raia wa Uganda wamepinga gharama ya kununua medali hizo ,wakisema fedha hizo zitumike katika sekta kama vile za afya,kulingana na The Monitor.

Tangazo hilo linajiri baada ya gazeti linalomilikiwa na serikali la New Vision kuripoti kwamba tume ya bunge ilitenga milioni 50 za Uganda ili kusimamia gharama za mazishi za wabunge.

Takriban wabunge 5 wamefariki katika kipindi cha miaka mitano iliopita.