Wanawake wajifunza kutumia teknolojia Kenya

Image caption Kulingana utafiti wa wakfu wa World Wide Web, ni 20% pekee ya wanawake katika vitongoji duni katika mji mkuu wa Nairobi wanaopata huduma za mitandao.

Kenya ni mojawapo wa mataifa barani Africa, ambapo asilimia kubwa ya raia wanapokea huduma za mitandao.

Hata hivyo, kulingana na utafiti wa wakfu wa World Wide Web, ni 20% pekee ya wanawake katika vitongoji duni katika mji mkuu wa Nairobi wanaopata huduma za mitandao.

Utafiti huo aidha umebaini kwamba 57% ya wanaume wanapokea huduma hizo.

Na huku ulimwengu ukiadhimisha wiki ya mitandao ya kijamii na teknolojia, mashirika mbalimbali yamejitokeza kupunguza pengo la kijinsia katika matumizi ya mitandao nchini Kenya.

Njia mbalimbali za ubunifu zinatumika kuwafunza wanawake.

Kiu ya elimu ya mitandao na teknolojia

Ndani ya kontena iliogeuzwa kwa ubunifu mkubwa na kuwa sawa na darasa ama Cyber cafe, masomo yanaendelea, ambapo wanawake walio na kiu cha kujua kutumia tarakilishi wamejitokeza.

Ndani ya kontena hiyo kuna wanawake 30 kutoka vitongoji mbalimbali katika kaunti ya Nairobi, mbele yao kuna vipakatalishi wanavyotumia kwa mafunzo, ambapo kwa baadhi ya wanawake hawa, wameona vipakatalishi kwa karibu kwa mara ya kwanza.

Mafunzo hayo yanatolewa katika maeneo tofauti nchini Kenya, kwani kontena hiyo inaweza kuhamishwa kwa urahisi.

Huwezi kusikiliza tena
Wanawake wajifunza kutumia teknolojia Kenya

"Nimekuja hapa kupata elimu ya tarakilishi, kwa sababu mimi ni 'analogue'. Anasema Demimah, mwanamke wa umri wa makamo.

Mradi huu unasimamiwa na kampuni ya kutengeneza tarakilishi, Intel, lengo likiwa kuwapa wanawake milioni moja nchini Kenya, mafunzo ya kimsingi kuhusu trakilishi na mitandao.

"Wanawake hawa wanatumiwa vibaya sana kwa sababu hawajui kutumia mitandao. Wanatoa pesa nyingi kupindukia kupata huduma ambazo wana uwezo wa kupata bila malipo." Diana Kwamboka, mmoja wa wakufunzi anasema.

Image caption Wanawake wanaopokea mafunzo ya kimsingi kuhusu tarakilishi na mitandao jijini Nairobi

Kwa wanawake hawa, umri sio hoja, bora tu wapate mafunzo ya kimsingi ya kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Tatizo liko wapi?

Kulingana na utafiti wa wakfu wa World Wide Web, jijini Nairobi, ni asilimia 20 pekee ya wanawake katika vitongoji duni wanaopata huduma za mitandao.

Istoshe, ni asilimia 25 pekee wanaoripotiwa kutafuta maelezo muhimu kuhusu haki zao. Tatizo liko wapi?

"Wanawake wengi wanaogopa teknolojia, pili hawajiamini vya kutosha kwamba wana uwezo wa kutumia teknolojia, pia hawana njia za kupata huduma za mitandao na mafunzo, na ndio sababu tunawapelekea huduma hizi waliko" Anasema Lavinia Muthoni, meneja wa mauzo wa kampuni ya Intel Africa mashariki.

Huwezi kusikiliza tena
Wanawake wajifunza kutumia teknolojia Kenya