Msongo wa mawazo watatiza wanajeshi wa zamani Kenya

Wanaharakati
Image caption Wanaharakati wameungana kuhamasisha umma kuhusu matatizo wanayopitia wanajeshi baada ya kutoka vitani

Msongo wa mawazo ni ugonjwa wa akili unaoweza kumuathiri mtu baada ya kushuhudia matukio kama vita, ambayo humfanya mtu kuishia kutumia vileo, kujihusisha na ghasia au hata pia kujitoa uhai.

Wanajeshi wa Kenya, wamekuwa katika maeneo yanayokumbwa na mizozo kama Somalia. Kumeendelea kuwa na shutuma kutoka kwa walio ndani ya jeshi na wengine nje, kwamba hakuna usaidizi wa kutosha kwa walioathiriwa kiakili kutokana na wanayo yashuhudia katika maeneo hayo ya mizozo.

Makundi tofuati ya umma, yameamua kuchukua hatua na kutoa usaidizi na uhamasisho kwa waathiriwa hao.

Byron Adera wa shirika la True North na pia afisa wa zamani wa kikosi maalum katika jeshi la Kenya, amelishuhudia tatizo hili katika miaka 8 aliyotumika kwenye jeshi.

Image caption Wanaharakati wakishiriki kampeni ya #22PushUp katika Mlima Longonot

"Tunaviita vidonda visivyoonekana. Kwa sababu kuna mambo yanayojitokeza katika namna zisizo za kawaida. Tumeskia wanajeshi wanaorudi nyumbani, ambao wanajiua, wanaua familia zao, wake zao. Mipango iliowekwa na watu wanaohusika moja kwa moja, yaani maafisa wa juu wa jeshi, au vikosi vya vita, kwa jumla haitoshi,'' anasema.

Kwa muda mrefu, jeshi la Kenya limekuwa katika maeneo yanayokumbwa na mizozo kama Somalia katika vita dhidi ya wanamgambo wa Al shabaab.

Hata hivyo duru kutoka ndani ya jeshi zinasema hakuna utaalamu wa kutosha kushughulikia idadi inayoongezeka ya wanajeshi wanaorudi kutoka maeneo hayo ya mizozo.

Ni vigumu kupata takwimu kuhusu ukubwa wa tatizo la msongo wa mawazo, na ukosefu wa ukaguzi una maana kuwa visa hivi hukosa kutambuliwa.

Ukweli huu umewashinikiza baadhi sasa kujaribu kuibadili hali.

Mzigo unaendelea kuilemea jamii na familia za walioathiriwa na msongo wa kimawazo ambao wengi wao hata hawafahamu kwamba wameathirika.

Huwezi kusikiliza tena
Msongo wa mawazo watatiza wanajeshi wa zamani Kenya

Cecelia Achola anakumbuka mumewe alivyobadilika aliporudi nyumbani kutoka vitani.

"Alivyobadilika alikuwa mlevi chakari...ilituathiri kabisa maanake mimi nilikuwa sifanyi kazi. Nilikuwa mke nyumbani, hakuna mtu wa kumtegemea, ilikuwa ni yeye tu ambaye pia anategemewa kwao. Kila mtu amkodolea macho, kuna shinikizo pia kazini," anasema.

"Sasa si atatafuta njia ya mkato? alewe aokotwe mahali atakapookotwa."

Mumewe Cecelia hatimaye aliamua kujiua.

Huku visa hivi vikikithiri, kundi la watoa ushauri nasaha limeamua sio tu kutoa ushauri huo bure, bali pia kuwawezesha wanajeshi kusaidiana.

Image caption Bi Susan Gitau

Mwanzilishi wa taasisi ya washauri nasaha ya International Professional Counsellors Susan Gitau anasema: '' Kunao wanaokuja na wale wanaojileta kivyao, na ni kwasababu tulifungua milango kama taasisi, hatahivyo sioni tukihudumu vilivyo, maanake najua kinachostahili kutendeka. Tungekuwa na mfumo moja wa kuwahudumia wanajeshi wetu. Hata kama tutauita Amisom KDF PTSD model ya Kenya, naona kuna kitu hatujafanya''.

Shutuma dhidi ya ukosefu wa jitihada za kutosha na taasisi za kukabiliana na magonjwa ya akili kwa wanajeshi zinazidi kuongezeka. Hadi pale hatua zaidi zitakapochukuliwa, Jinamizi linalowakabili wanajeshi hawa litazidi kuwaandama.

BBC imewasiliana na idara ya jeshi nchini Kenya, lakini haikufanikiwa kupata kauli kuhusu suala hili.