Rais Rodrigo Duterte aliamuru kuuawa kwa wanasiasa waliompinga

Duterte alikuwa Meya wa Davao mwaka 1988 Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bw Duterte alikuwa Meya wa Davao mwaka 1988

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, aliamuru kuuawa kwa wanasiasa wapinzani alipokuwa meya wa zamani wa Davao, mwanachama mmoja wa kikosi kilichopewa jukumu la kuwaua walanguzi wa biashara haramu ya mihadarati, amesema.

Edgar Matobato ameiambia kamati ya bunge la seneti kwamba yeye na wauaji wenzake, wamewaua zaidi ya watu 1,000 katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Alielezea kwa kina, namna genge hilo lilipokuwa likitekeleza mauaji hayo ya kutisha dhidi ya washukiwa wa mihadarati, huku akitoa kisa cha kinyama pale walipomchukua mhasiriwa mmoja na kumlisha kwa mamba.

Msemaji wa Bwana Duterte amepinga madai hayo, huku akisema kwamba, uchunguzi kuhusiana na mamlaka ya Duterte akiwa meya, hauendi popote.

Bw Matobato, mwenye umri wa miaka 57, amesema kuwa alikuwa mwanachama wa Davao Death Squad, kundi moja baya la kiusalama, linalodaiwa kuhusika na mamia ya mauaji.

"Kazi yetu ilikuwa kuwaua wahalifu kama wauzaji dawa za kulevya, wabakaji, wanyang'anyi na kadhalika," alisema.

Wapinzani kuuawa

Pia amedai kuwa wapinzani wa kisiasa wa Bw Duterte, walilengwa, wakiwemo walinzi wanne wa mwaniaji mmoja wa kiti cha umeya mjini humo, Prospero Nograles.

Waathiriwa walipigwa risasi au kunyongwa, huku baadhi ya wengine wakipasuliwa na kutolewa matumbo na kisha kutupwa baharini ili kuliwa na samaki.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Edgar Matobato akizungumza katika kikao cha kamati ya senate

Aliambia kikao cha bunge la seneti, kwamba alitoka katika mpango wa kuwalinda mashahidi na kukimbilia mafichoni, baada ya Bw Duterte kuwa Rais, huku akihofia maisha yake.

Aidha Bw Matobato amedai kuwa Duterte aliamuru kulipuliwa kwa msikiti mmoja kama jibu la shambulio dhidi ya kanisa la Davao Cathedral mwaka 1993.

Katika madai yake, msemaji wa Bw Duterte, amesema "sidhani ana uwezo wa kuamrisha hayo".

Mwanawe Prospero Nograles, Karlo, mwaakilishi wa mji wa Davao, amekanusha madai ya Bw Matobato kuhusiana na mauaji ya walinzi wa babake.

"Sielewi kabisa asemacho mtu huyu".

"Naweza tu kushuku kuwa mtu huyu anatumika na baadhi ya watu, ili kutimiza maslahi ya ubinafsi," aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Facebook.

Bw Duterte alikuwa meya wa mji wa Davao mnamo mwaka 1988, na msimamo wake mkali ulishuhudia kushuka pakubwa kwa uhalifu, hatua ambayo ameiendeleza kwenye taifa nzima.

Tangu kuchaguliwa kwake mwaka huu zaidi ya watumizi na walanguzi wa mihadarati wapato 3,000 wameuawa licha ya kuwepo kwa kilio kutoka mataifa ya dunia kuhusiana na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Lakini Bw Duterte amepuuzilia mbali vilio hivyo na kutetea sera hiyo yake, huku akimtaja katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kama "mjinga" na kumuita Rais wa Marekani Barack Obama "mwana wa kahaba", matamshi ambayo baadaye alisema kuwa amejutia.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii