UN yakasirishwa na ucheleweshwaji wa misaada ya kibinaadam Syria

Kumekuwa na uhaba wa chakula na huduma muhimu sehemu za mapigano
Image caption Kumekuwa na uhaba wa chakula na huduma muhimu sehemu za mapigano

Maafisa wa umoja wa mataifa wameonyesha hasira juu ya kushindwa kwao kusambaza misaada ya kibanadamu huko Syria, licha ya usitishwaji wa mapigano kuanza tangu siku ya jumatatu.

Mjumbe maalum wa umoja wa mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura amesema kuwa serikali ya nchi hiyo haijatoa kibali cha kuruhusu usambazaji wa misaada kama walivyoahidi, huku mshauri wa masuala ya kibinadamu Jan Egeland anawashutumu waasi huko Aleppo kwa kucheza mchezo wa kisiasa.

Washirika wakuu wa Rais Assad, Urusi wamesema kuwa vikosi vya serikali vimeondoka katika barabara kuu ya kuelekea mji wa kaskazini mwa Aleppo, hii ikimaanisha kuwa msafara wa misaada wa umoja wa mataifa unaweza kufika katika maeneo yaliyoshikiliwa na waasi siku ya leo.

Lakini Marekani inasema kuwa haina uhakika kama kuondoka huko kumeanza.