Uingereza yaomba radhi kifo cha mvulana wa Iraq

Ahmed Jabbar Kareem Ali
Image caption Ahmed Jabbar Kareem Ali alifariki kwenye mfereji wa maji Basra 2003

Wizara ya ulinzi ya Uingereza imeomba radhi kutokana na kifo cha mvulana wa Iraq ambaye aliachwa kufa maji mjini Basra mwaka 2003.

Mvulana huyo Ahmad Ali alikuwa miongoni mwa raia wanne wa Iraq waliokuwa wamekamatwa na wanajeshi wa Uingereza kwa tuhuma za uporaji.

Kama adhabu, walilazimishwa kuingia kwenye mfereji uliojaa maji.

Ahmad Ali, ambaye hakujua kuogelea, alikufa maji.

Wanajeshi waliohusika katika kisa hicho waliondolewa makosa ya kuua bila kukusudia mwaka 2006 na mahakama ya kijeshi lakini ripoti mpya imeibuwa maswali kuhusu vitendo vyao.

Kisa hicho kilikuwa miongoni mwa visa vya vifo vya raia, vilivyotokea wakati wa uvamizi wa nchi za magharibi ulioongozwa na Marekani nchini Iraq kati ya mwaka 2003 na 2011, ambavyo vimekuwa vikichunguzwa.

Ripoit ya jaji aliyechunguza kifo cha Ahmed amesema mvulana huyo hakufaa kabisa kuzuiliwa na pia hakufaa kushurutishwa kuingia kwenye mtaro.

Aidha, amesema wanajeshi hao walifaa kumuokoa walipoona anatatizika majini.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Mji wa Basra ulikuwa umetawaliwa na vurugu wakati huo, ripoti hiyo ya uchunguzi inasema

Ayad Salim Hanoon, mmoja wa watu wengine waliozuiliwa na wanajeshi wa Uingereza, amesema wanne hao walilazimishwa kuingia kwenye maji ya mtaro wa Shatt-Al Basra wakiwa wameelekezewa mtutu wa bunduki.

Rais Saddam Hussein aliondolewa mamlakani na majeshi ya nchi za Magharibi katika operesheni iliyosababisha vifo vya raia 150,000 wa Iraq na wengine zaidi ya milioni moja kuachwa bila makao.