Aliyeigiza Liesl The Sound of Music Charmian Carr afariki dunia

Charmian Carr in 2012 Haki miliki ya picha Getty Images

Mwigizaji Mmarekani Charmian Carr, aliyeigiza binti mkubwa wa familia ya von Trapp Liesl katika filamu ya The Sound of Music iliyozinduliwa mwaka 1965, amefariki dunia akiwa na miaka 73.

Carr amefariki akiwa mjini Los Angeles baada ya kupata matatizo kutokana na aina nadra ya ugonjwa wa dementia, mwakilishi wake amesema.

Akiigiza kwenye filamu hiyo maarufu sana ya mwaka 1965, alisifika kwa alivyoimba wimbo wa Sixteen Going on Seventeen.

Baada ya kuondoka kwenye ulingo wa filamu, alianzisha biashara ya kupamba nyumba katika jimbo la California.

Mamake ndiye aliyempangia kwenda kushindania nafasi ya kuigiza Liesl, ingawa hakuwa amepokea mafunzo ya uimbaji au uigizaji.

Filamu hiyo ya The Sound of Music iliyondaliwa na Rodgers na Hammerstein ilivuma sana, na iliipiku filamu ya Gone with the Wind wakati huo na kuwa filamu iliyozoa kitita kikubwa zaidi cha pesa katika historia kufikia wakati huo.

Image caption Kym Karath aliigiza kama binti mdogo zaidi Gretl katika filamu hiyo

Carr baadaye aliandika vitabu viwili kuhusu aliyopitia, Forever Liesl (Daima Liesl) na Letters to Liesl (Barua kwa Liesl), na alitokea mara kwa mara katika hafla za kuadhimisha filamu hiyo.

Kushiriki kwake pakubwa katika uigizaji ilikuwa ni katika filamu ya televisheni ya Stephen Sondheim kwa jina Evening Primrose.

Liesl halisi, Agathe von Trapp, mwaka 1946

Wengi wa mashabiki wa The Sound of Music wamekuwa wakituma salamu za rambirambi kwenye Twitter na pia kupakia sehemu alizoigiza Carr kwenye filamu ya The Sound of Music.

Kym Karath, aliyeigiza kama Gretl kwenye filamu hiyo, ameandika kwenye Twitter: "Amekuwa kama dadangu maisha yangu yote."

Haki miliki ya picha AP
Image caption Agathe von Trapp (wa pili kutoka kushoto) akifanya mazoezi na Trapp Family Singers mwaka 1946

Liesl halisi, Agathe von Trapp, binti mkuwa wa familia ya von Trapp iliyotoka Austria, alifariki mwaka 2010 akiwa na umri wa miaka 97.