Kesi ya Somalia na Kenya yasikizwa mahakama ya UN, Uholanzi

Bahari Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Eneo linalozozaniwa linakakisiwa kuwa na mafuta na gesi

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeanza kusikiliza kesi ya mzozo wa mpakani kati ya Kenya na Somalia.

Kesi hiyo inasikizwa mjini The Hague, Uholanzi.

Mataifa hayo yanazozana kuhusu mpaka katika Bahari ya Hindi.

Mwanasheria mkuu wa Kenya Prof Githu Muigai amesema anaongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa maafisa kutoka Kenya kutetea taifa hilo.

Kupitia taarifa, anasema Kenya inaituhumu Somalia kwa kuvunja mkataba wa mwaka 2009 ambapo anasema nchi zote mbili ziliafikiana kutatua mzozo huo kupitia mazungumzo.

Mwenzake wa Somalia Ahmed Ali Daahir amesisitiza kuwa mahakama ICJ ndiyo yenye mamlaka ya kuamua tofauti hiyo baada ya bunge la taifa la Somalia kupinga mkataba huo wa 2009.

"Kwa hakika tunaamini kuwa tutapata haki yetu katika mahakama ya ICJ. Tuamini kuwa mahakama hiyo inauwezo wa kusikiza kesi hiyo ya kimataifa na kutoa kauli itakayoheshimiwa na mataifa haya mawili. Tuna matumaini makubwa kuwa kauli ya mahakama hii itatupatia sehemu hiyo ya mpakani ndani ya bahari hindi," ameambia BBC.

Eneo linalozozaniwa baharini ni la ukubwa wa zaidi ya kilomita 42,000 mraba.

Uchunguzi umeonesha eneo hilo huenda likawa na gesi.

Mzozo huo umesababisha wawekezaji kutoangazia zaidi eneo hilo kutokana na ukosefu wa habari kamili kuhusu nani mmiliki wa mafuta na gesi ambavyo huenda vikagunduliwa eneo hilo.

Kenya tayari imetoa kandarasi kwa kampuni za kigeni kufanya upepelezi wa kutafuta mafuta na gesi eneo hilo.

Somalia inataka mpaka wa baharini uendelee kwa kufuata mstari wa mpaka ulio nchi kavu ukielekea kusini mashariki lakini Kenya inataka mpaka huo uwekwe kwa kufuata mstari usiopinda unaoelekea mashariki.

Hili limesababisha kuwepo kwa mzozo kuhusu sehemu ya bahari ya umbo la pembe tatu.

Vikao vya mahakama wiki hii ni vya kuamua iwapo kesi hiyo inafaa kusikizwa na kuamuliwa na mahakama hiyo.

Somalia iliwasilisha kesi hiyo katika mahakama ya ICJ Agosti 2014. Kwenye nyaraka zake, serikali ya Somalia ilisema juhudi za kutatua mzozo huo kwa njia za kidiplomasia

Kenya iliwasilisha ombi la kupinga kukubaliwa kwa kesi hiyo Oktoba mwaka 2015. zilikuwa zimegonga mwamba.