Ethiopia yaomba msamaha kuhusu makosa kwenye vitabu

Ramani ya taifa la Ethiopia
Image caption Ramani ya taifa la Ethiopia

Wizara ya Elimu nchini Ethiopia imeomba msamaha kufuatia makosa yaliyochapishwa katika vitabu kadhaa vya shule.

Makosa hayo yanahusiana na mipaka ya majimbo nchini humo.

Wizara hiyo inasema wanafunzi na waalimu walipotoshwa kutokana na vitabu hivyo vilivyochapishwa mwaka wa 2004 na 2010.

Ethiopia kwa sasa inakabiliwa na maandamano ya kuipinga serikali katika majimbo yake mawili makubwa zaidi.

Katika mojawapo ya makosa hayo, mlima mrefu zaidi nchini humo Ras Dashen umewekwa katika jimbo la Tigray na sio Amhara ambapo mlima huo upo.

Kulingana na mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza vitabu hivyo pia havionyeshi mipaka sawa ya majimbo mengine.

Makosa hayo yaliwekwa wazi kwa mara ya kwanza katika habari kwenye runinga ya kitaifa.

Wanaharakati wa upinzani wanasema hatua hiyo ilikuwa makusudi na inaonyesha kuendelea kwa serikali kujaribu kubadili historia ya nchi hiyo.Haijabainika iwapo vitabu hivyo vitaondolewa.

Ombi hilo la msamaha linawadia huku Ethiopia ikikabiliwa na maandamano ya kuipinga serikali katika majimbo ya Oromia na Amhara ambayo ni makubwa zaidi nchini humo.

Mwezi Julai, maandamano yalizuka katika maeneo ya Kaskazini baada ya serikali kukosa kubadili usimamizi wa eneo moja kutoka Tigray hadi Amhara kama waakaazi wa eno hilo wanavyotaka.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanasema zaidi ya watu mia tano wameuawa nchini humo tangu mandamano hayo kuzuka upya mwezi Novemba mwaka jana.