Kisiwa ambacho wanawake huwabeba wanaume Rwanda

Baadhi ya wanawake katika kisiwa cha Nkombo, Rwanda
Image caption Baadhi ya wanawake katika kisiwa cha Nkombo, Rwanda

Katika kisiwa Nkombo, kilichopo magharibi mwa Rwanda katika ziwa Kivu, kuna utamaduni wa kipekee usiokuwepo popote pale nchini Rwanda ambapo wanawake huwaosha miguu waume zao, kuwapaka mafuta na kuwabeba mgongoni hadi kitandani.

Wanawake walioozungumza na BBC wanasema utamaduni huo sio kudhalilisha mwanamke wala mke kunyenyekea mmewe kupindukia bali ni kuonesha upendo.

Wanaume wanasifia sana utamaduni huo kiasi kwamba baada ya ndoa hutoa mahari tena mara nyingi iwezekanavyo.

"Bwana anaporudi nyumbani anakuta umechemsha maji. Unamuosha miguu na kumpaka mafuta...kwa kuwa kawaida huwa amechoka, unamweka mgongoni hadi kitandani, Josephine Nyirantibashima aliambia mwandishi wa BBC Yves Bucyana.

"Mimi binafsi mzee wangu ana miaka 51 na mimi nina 48 nampa huduma hiyo."

Image caption Bi Nyirantibashima Josephine

Yeyote unayemuuliza katika kisiwa hiki anakusimulia jinsi anavyobeba au kubebwa mgongoni na mme au mkewe:

Rurangwa Jean Damascene ni miongoni mwa wanaume wanaodai kuonja kile wanachotaja kuwa utamu wa utamaduni huo.

"Mimi kila mara nikienda bafuni mke wangu huwa ananisaidia kunisafisha. Sijamlazimisha. Yeye mwenyewe anafanya hivyo kwa moyo wake mkunjufu," anasema.

"Hata kunibeba mgongoni hadi kitandani nikalala na kusinzia vizuri sana. Hufanya hivyo mara nyingi. Unajua? Kuna wakati mtu anakuwa amechoka sana. Kwa hiyo hapa kwetu siyo ajabu kabisa."

Wanawake katika kijiji hicho waliambia BBC kwamba kuwabembeleza waume zao siyo kwamba wananyenyekea kupindukia wala kuwaogopa waume zao.

Image caption Wanaume wanasifia sana utamaduni huo kiasi kwamba baada ya ndoa hutoa mahari tena mara nyingi iwezekanavyo.

"Mfano mimi nyumbani tuna tatizo la uhaba wa chakula baada ya mamlaka kufunga shughuli za uvuvi katika ziwa Kivu,bwana hana kazi kwa sasa, lakini pamoja na hayo nitajitahidi kumliwaza. Lazima nimbebe mgongoni, siwezi kwenda kinyume na utamaduni huo ili na yeye asisite kutoa mahari kwetu mara kadhaa," alisema mmoja wao.

Mahari anayozungumzia yanatolewa na mwanaume hata baada ya ndoa kama ishara ya kuridhika na ndoa yake.

"Alitoa mahari kwetu mara nne pekee kwa sababu uwezo wake siyo mkubwa. Lakini bwana kutoa mahari mara kadhaa nyumbani kwa mkewe kunatokana na utamaduni wetu wa namna tunavyowabembeleza waume zetu. Kawaida huwezi kuolewa bila bwana kutoa mahari,lakini hata baada ya kuolewa anatoa mahari mara kadhaa kubainishia familia ya mkewe kuwa walilea vizuri."

Rwanda ni miongoni mwa nchi zilizo mstali wa mbele katika swala la usawa wa jinsia na kuwajali sana wanawake.

Je utamaduni huu waweza kuchukuliwa kama ukandamizaji wa wanawake?

Wakuu wa makundi ya kidini katika kisiwa hiki wanasema hili ni suala la utamaduni wa wananchi.

Hanyurwa Jean ni mchungaji wa la Kiangilikana: "Tunapofundisha bi harusi na bwana harusi watarajiwa hapa kanisani wanatuambia kinagaubaga kuwa huu ni utamaduni wao. Sio swala la wanawake kulinda ndoa zao zisivunjike, hapana!."

Huwezi kusikiliza tena
Kijiji ambacho wanawake 'huwabeba wanaume' Rwanda

"Pia sidhani kwamba utamaduni huu unakinzana na masharti ya usawa wa jinsia, hapana! Utamaduni huu haujawakataza kuheshimiana na kushirikiana kama mke na mme. nionavyo ni swala la utamaduni kuliko tunavyofikiria kwamba wanawake wanaogopa waume zao. Huwezi kuwakataza kufanya hivyo? Ni kama uwakataze kuzungumza lugha zao asilia."

Maafisa wa serikali wanasema wanawake kuwabeba waume zao mgongoni siyo utamaduni unaofaa kwa wakati huu lakini kwamba ni vigumu kumkataza mtu anachokitaka.