Obama ayataka mataifa tajiri kusaidia wakimbizi

Mkimbizi wa Syria Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mkimbizi wa Syria

Rais wa Marekani Barack Obama ameyataka mataifa tajiri kufanya kila linalowezekana kuwasaidia watu wanaokimbia vita.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano kuhusu wakimbizi katika Umoja wa Mataifa amekiri kuwa dunia inakabiliwa na changamoto nyingi.

Amezitaka nchi tajiri kuchukulia tatizo hilo kama ni la kwao na kuongeza kuwa tatizo la sasa la wakimbizi ni ishara ya vita na mateso na kwamba itaweza kushughulikiwa tu endapo migogoro kama ule wa Syria utamalizwa.

Aidha amezitaja nchi 50 zinazoshiriki mkutano huo kuwa zimeahidi kuchukua wakimbizi laki tatu na sitini elfu katika kipindi cha mwaka huu, ikiwa ni mara mbili ya idadi ya mwaka uliopita, huku Canada na Ujerumani zikiongoza.

Rais Obama pia ametangaza kwamba fedha zilizokuwa zikichangwa na mashirika ya kibinadamu na Umoja wa Mataifa zimeongezeka kwa dola ya Marekani bilioni nne nukta tano.