Binadamu kupandikizwa kichwa 'kufikia 2017'

Upandikizaji kichwa Haki miliki ya picha Thinkstock

Daktari wa upasuaji anayetaka kufanya upandikizaji wa kwanza wa kichwa kuwahi kufanyika anasema upasuaji huo unaweza kufanyika kuanzia mwaka ujao.

Prof Sergio Canavero ameiambia BBC amepata watu kadhaa kutoka Uingereza waliojitolea kufanyiwa.

Upasuaji huo utahusisha kichwa cha mgonjwa kubandikwa katika mwili wa mtu aliojitolea.

Licha ya kuwa ni taswira ya kuogofya, Prof Canevero ana imani kwamba sasa teknolojia hiyo inaweza kufanikishwa.

"Itategemea lakini iwapo kutapatikana mtu wa kufaa atakayejitolea ubongo.

"Ilichukuwa miezi kadhaa kufanikisha upandikizaji wa mwisho wa uso uliofanyika, kwasababu hapakuwa na mtu wa kufaa aliyejitolea, lakini teknolojia itakuwepo." Canavero ameiambia BBC.

Haki miliki ya picha Facebook
Image caption Prof Canavero hatofanya tena majaribio kwa kutumia ndizi

Licha ya hatari kubwa katika upasuaji huo, Dakatari huyo anasema amepata watu wengi waliojitolea kufanyiwa upandikizaji huo.

Mgonjwa

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Valery Spiridonov anataka kufanyiwa upandikizaji wa kichwa

Valery Spiridonov ana miaka 31 na anaugua tatizo la kulika misuli, lililomsababisha kuishia kwenye kiti cha magurudumu.

Akizungumza kwenye televisheni ya ITV Uingereza, anasema yuko radhi kichwa chake kipandikizwe kwenye mwili tofuati.

"Maisha yangu leo ni magumu, na ninategemea mno watu kunisaidia kila siku - saa nyengine hata mara mbili kwa siku, kwasababu nahitaji mtu anitoe kitandani, na aniweke kwenye kiti.

"Inanifanya ninategemea watu sana.

"Iwapo kuna namna ya kulibadili hili, naamini tunapaswa kujaribu na kuitumia njia hiyo."

Vipi upandikizaji wa kichwa utakavyofanikishwa?

Daktari anadai upandikizaji huo utahitaji wahudumu 150 wa afya, na saa 36 kufanya upasuaji huo.

Anasema hatua ya kwanza itakuwa ni kukigandisha kichwa na mwili kuuzuia mwili usife.

Baada ya hapo shingo itakatwa na mipira iunganishwe na mishipa tofuati ya mwili.

Alafu inawadia sehemu iliyo ngumu,, kuukata uti wa mgongo. Utakatwa na kisu maalum kilichotengenezwa kwa almasi kutokana na nguvu za jiwe hilo.

Baadaye kichwa kinaunganishwana mwili na uti wa mgongo unashikanishwa pamoja kwa gundi maalum.

Misuli, mishipa na sehemu za ndani ya mwili zinarudishwa na ngozi inashonwa upya.

Kuifanyia Sayansi majaribio

Haki miliki ya picha Thinkstock

Profesa Canavero anasema kutakuwa na majaribio kwa watu waliojitolea walio na ubongo usio fanya kazi.

Wataalamu wengi wa afya wanasema uvumbuzi wake hauna uhalisi na upandikizaji wa kichwa hauwezekani kabisa.

Lakini Profesa Canavero ameiambia BBC kuwa ana imani anaweza kufanikisha upasuaji huo.

Profesa Canavero anasema 90% ina maana kuwa mgonjwa atainuka pasi kuwa na madhara yoyote na ataweza kutembea katika muda wa mwezi mmoja.

Kwa sasa anasema lengo lake ni kuleta matumaini kwa watu waliovunjwa moyo na madawa ya mataifa ya magharibi.