Tanzania yapokea ndege mpya kutoka Canada

Ndege hiyo mpya ikipata saluti ya maji kutoka kwa magari ya Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Tanzania mara tu bada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere 20 Septemba Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania
Image caption Ndege hiyo mpya ikipata saluti ya maji kutoka kwa magari ya Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Tanzania mara tu bada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere

Tanzania imepokea ndege mpya ya kutumiwa na Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) katika hatua ambayo inatarajiwa kuimarisha safari za ndani ya nchi za shirika hilo.

Ndege hiyo aina ya Bombadier Q400 NextGen ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA) kutoka Canada ilikotengenezewa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamriho aliambia wanahabari kwamba ndege ya pili inatarajiwa kuwasili baada ya wiki moja.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 76 ilianza safari ya kuelekea Tanzania wiki mbili zilizopita ikiwa na ikiwa na marubani wanne.

Ilipitia miji ya Reykjavík, Southampton, Malta, Luxor na Addis Ababa Ethiopia.

Rais Magufuli alikuwa ameahidi kwamba shirika hilo lingeimarishwa na ndege mpya kununuliwa mara baada ya kuingia madarakani.

Ndege hizo mbili zinatarajiwa kuanza safari zake baada ya kukamilisha mchakato wa kusajiliwa na Mamlaka ya Usalama wa Anga Tanzania (TCAA).

Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania
Image caption Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 70

"Kwa kuwa zitakuja zikiwa na usajili wa nchini Canada, tutalazimika kutumia siku mbili hadi tatu kuziingiza kwenye usajili wa TCAA pamoja na kukamilisha taratibu nyingine za kisheria ili ziweze kupata ruhusa ya kufanya safari za hapa kwetu," maafisa wa ATCL walikuwa wametangaza awali, kwa mujibu wa gazeti la Habari Leo.

Safari ya kwanza ya ndege hiyo, inatarajiwa kufanyika Septemba 27, mwaka huu kwenda jijini Mwanza.

Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania

Baadhi ya maeneo ambayo ATCL inatarajia kuongeza safari zake ni Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Bukoba na Visiwa vya Comoro.