Wanaoitumia vibaya bendera Zimbabwe kuadhibiwa

Mchungaji Evans Mawarire aliitumia bendera katika maandamano ya kupinga serikali Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mchungaji Evans Mawarire aliitumia bendera katika maandamano ya kupinga serikali

Waziri wa haki Zimbabwe ameonya yoyote anayeuza au kutumia bendera ya taifa bila ruhusa kuwa atashtakiwa kwa kuishusha hadhi heshima yake.

Onyo la Virginia Mabhiza linajiri baada ya bendera hiyo kutumika kama ishara ya maandamano ya kuipinga serikali mwezi Aprili wakati Mchungaji Evan Mawarire aliweka kanda yake ya video akilalamika kuhusu kuzidi kudorora kwa uchumi wa taifa linaloongozwa na rais Robert Mugabe tangu uhuru 1980.

Katika taarifa amesema, wahalifu watafungwa kwa hadi miezi 6 gerezani au kutozwa faini ya $200 au kukabiliwa na adhabu zote mbili kwa mara moja.

Bi Mabhiza ameongeza:

''Raia yoyote wa umma atakayejihusisha na shughuli zozote zinazohusisha utengenezaji, uuzaji au kuitumia bendera ya taifa kinyume na sheria, wameonywa kuanzia sasa kwamba wanaweza kushtakiwa na wanaweza kufungwa iwapo watapatikana na hatia mahakamani."