Utata DRC; wapinzani wadai ratiba ya uchaguzi wa mwaka huu

Waandamanaji wamekuwa wakishinikiza uchaguzi ufanyike mwaka huu kwa mujibu wa katiba ya DRC
Image caption Zogo kuhusu kutokuwepo kwa raiba ya uchaguzi DRC

Serikali ya Jamhuri ya Kidemocrasi ya Congo imesimamisha rasmi majadiliano baina yao na viongozi wa upinzani huku harakati za maandamano zikiwa zingali zinafukuta kushinikiza kwamba maandalizi yauchaguzi unaotarajiwa kabla ya mwishoni mwa mwaka, yafanyike kwa wakati.

Majadilano hayo ambayo tayari yalikuwa yameanza mwanzoni mwa mwezi yanasusiwa na baadhi ya vyama vikuu vya upinzani nchini huko kikiwemo kile cha mmojawapo ya mwanasiasa mongwe nchini humo, Etienne Tshisekedi, wa chama cha UDPS.

Mazungumzo hayo yalikuwa yamependekezwa na serikali baada ya wanaharakati wa upinzani kuitaka serikali itoe ratiba kamilifu ya jinsi uchaguzi huo utakavyofanyika.

Kufikia Disemba mwaka huu Rais Joseph Kabila, atakuwa ameshahudumu mihula miwili anayo ruhusiwa kwa mujibu wa katiba ya nchini hiyo .

Hata hivyo tume ya uchaguzi nchni humo inasema kulingana na mazingira yalivyo sasa ni vigumu kuandaa kabla mwaka huu kumalizika.

Tume hiyo ilikuwa inatarajiwa kutangaza tarehe ya uchaguzi hapo jana , lakini hilo halikufanyika.

Ndipo polisi walipokabiliana na waandamanaji waliokuwa wakishinikiza kutolewa kwa ratiba hiyo huko mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa, na kusababisha watu kadhaa kuuawa.

Duru tofauti zinahitilifaina kuhusu idadi ya watu waliouawa huku zingine zikiripoti hadi watu 50.