Wachina wadukua programu ya gari la umeme la Tesla

Gari la Tesla
Image caption Gari la Tesla

Kampuni ya Tesla imeimarisha programu yake baada ya watafiti kutoka China kudukua mfumo wa uendeshaji wa gari hilo.

Kundi hilo kutoka kampuni ya usalama ya Keen Security Lab lilingilia programu ya breki za gari hilo wakati ilipokuwa ikiendeshwa katika umbali wa kilomita 19.

Wakitumia laptopu ,wadukuzi hao pia walifanikiwa kufungua mlango wa gari hilo bila kutumia funguo.

Tesla imelazimika kuimarisha programu yake ili kuzuia wadukuzi wengine kuingilia kati.

Udukuzi huo ulifanyika baada ya miezi kadhaa ya utafiti na kundi hilo la Keen Security Lab lilichapisha video za juhudi zake katika mtandao wa Yutube mapema wiki hii.

Wakati wa Udukuzi huo, mmoja ya wadukuzi alilidhibiti gari hilo kutoka kwa kiti cha abiria wakati ambapo dereva alikuwa akibadilisha barabara.