Wamarekani waandamana kupinga mauaji ya mtu mweusi

Waandamanaji Marekani Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maandamano Marekani

Maandamano yamezuka kwa siku wa pili mfululizo katika mji wa Charlotte, Marekani, kufuatia kifo cha mtu mmoja mweusi aliyepigwa risasi na polisi, Jumanne usiku.

Polisi wa kuzuia ghasia wametumia mabomu ya machozi kutawanya umati mkubwa wa watu wenye hasira waliokuwa wamekusanyika katikati ya mji.

Katika ghasia hizo mtu mmoja aliuawa kwa risasi.

Serikali katika eneo hilo imeyaita mauaji hayo kama ya raia kwa raia.

Maandamano na Ghasia zilizuka Jumanne usiku baada ya polisi kumuua Keith Lamont Scott, huku wakisema kwamba kijana huyo alikuwa na bunduki na kwamba alipuuza wito wa kuweka silaha chini.

Hata hivyo familia ya kijana huyo imesema kuwa hakuwa amebeba silaha yoyote

Meya wa mji huo, Jennifer Roberts, ameiambia BBC kuwa aliwataka polisi kumwonyesha mkanda wa video ya tukio hilo.