Al-Shabab lakiri kuvamia kituo cha polisi Kenya

Wapiganaji wa kundi la al-Shabab
Image caption Wapiganaji wa kundi la al-Shabab

Kundi la wapiganaji wa alshabab limekiri kuhusika na shambulio la kituo cha polisi kaskazini mwa Kenya karibu na mpaka na Somalia.

Baadhi ya wakaazi wameripoti kwamba maafisa wawili wa polisi walijeruhiwa katika shambulio hilo katika eneo la Hamey ambalo haliko mbali na mji wa Garissa na wengine wengi hawajulikani waliko.

Uvamizi huo ulifanyika saa sita ya usiku wa kuamkia Alhamisi

Msemaji mmoja wa kundi hilo ameiambia BBC kwamba wavamizi hao waliwaua maafisa sita wa polisi na kuwateka nyara wengine wawili.

Wapiganaji hao walifanikiwa kukiteka nyara kituo hicho baada ya maafisa wa polisi kutoroka,kundi hilo limesema.

Gari moja pamoja na silaha ziliibwa.

Mwandishi mmoja mwenye makao yake wilayani Dadaab amesema kuwa afisa mmoja wa polisi aliyejeruhiwa katika shambulio hilo kwa sasa anapata matibabu.

Kundi la wapiganaji wa al-Shabab lilifanya mashambulio kadhaa nchini Kenya ikiwemo lile la mauaji ya Chuo kikuu cha Garissa mnamo mwezi Aprili 2015 ambapo takriban watu 147 waliuawa.