Makombora ya Muungano wa Saudia yawaua 19 Yemen

Afisa wa serikali Yemen anasema huenda makaazi ya watu yalilengwa 'kimakosa' Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Afisa wa serikali Yemen anasema huenda makaazi ya watu yalilengwa 'kimakosa'

Raia 19 wameuawa katika mji wa bandari wa Hudaydah nchini Yemen kwenye mashambulio ya muungano unaoongozwa na Saudia, maafisa wa eneo hilo na wahudhumu wa afya wanasema.

Uvamizi wa jumatano unaarifiwa kulenga kasri la rais linalotumika na waasi wa Houthi lakini makombora yalilenga nyumba zilizokaribiana na kasri hilo.

Wakaazi wameilezea uharbifu mkubwa uliotokea katika wilaya ya al-Hunoud.

Muungano huo, unaotaka kuirudisha uongozini utawala unatoambulika kimataifa ya Yemen, bado haujatoa kauli.

Maafisa wa muungano huo wanasema hulenga maeneo ya kijeshi pekee, lakini umeshutumiwa kwa kulenga shule, hospitali, masoko na makaazi ya watu tangu kuingilia kati mzozo wa Yemen miezi 18 iliopita.

Shirika la habari la Saba linalodhibitiwa na waasi limeripoti kuwa nyumba kadhaa ziliharibiwa katika shambulio hilo la Hudaydah.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hali imekuwa mbaya Yemen na watu wengi wanahitaji usaidizi wa kibinaadamu

Imetaja wahudumu wa afya waliosema kuwa kuna watu 98 waliofariki wakiwemo wanawake na watoto.

"kulikuwa na uharibifu mkubwa. Sehemu za mwili zimechangika na masalio ya nyumba zilizoporomoka na damu imetapakaa kila mahali," mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la Reuters.

Afia wa serikali ameliambia shirika la AFP kwamba eneo hilo la makaazi huenda limelengwa 'kimakosa'.

Umoja wa mataifa unasema zaidi ya watu 6, 700 wameuawa tangu kuanzishwa kwa kampeni ya kijeshi inayomuunga mkono rais Abdrabbuh Mansour Hadi Machi 2015, miezi mitatu baada ya waasi kuudhibiti mji mkuu, Sanaa.

Mzozo huo pia umeisukuma nchi hiyo masikini katika mataifa ya kiarabu karibu kuingia kwenye baa la njaa na kusababisha 80% ya idadi ya watu nchini humo kuhitaji usaidizi wa kibinaadamu.