Polisi Sierra Leone wamuachia huru mtuhumiwa wa ukeketaji

'Kwanini ukeketaji?' picha Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wanaharakati wameshinikiza kampeni kubwa ya kusitisha utamaduni huo Afrika

Polisi nchini Sierra Leone wamemuachia huru mwanamke anayetuhumiwa kutekeleza ukeketaji kufuatia shinikizo kutoka kundi lenye ushawishi katika jamii la wakeketaji.

Elsie Kondoromoh "aliachiliwa kwa muda" baada ya wakeketaji wengi kulalamika dhidi ya kukamatwa kwake, Inspekta wa polisi Marty Tarawallie amesema.

Wakeketaji wengine waliobeba vijiti waliandamana pia katika hospitali alikolazwa anayetuhumiwa kuwa muathiriwa.

Ukeketaji upepigwa marufuku kwa sasa Sierra Leone.

Marufuku hiyo imeidhinishwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika eneo hilo mnamo Desemba 2013, na kusababisha vifo vya watu 11,000.

Lakini ukeketaji wa wasichana ambao baadhi wanaona kama utamaduni wa kubaleghe, umefufuliwa katika miezi ya hivi karibuni.

Wanaharakati wengi wanashutumu maafisa wa serikali kwa kushindwa kusitisha ukeketaji kutokana na nguvu walionayo katika jamiiwakeketaji.

'Afungwa macho'

Khadija Balayma Allieu, mwenye umri wa miaka 28, anasema alifungwa macho na kubururwa katika chumba kimoja nyumbani Kenema na hadi wakeketaji 6.

"mmoja aliniketia kifuani, wawili walinizuia mikono na wengine wawili walinishikilia miguu wakaipanua. Waliniziba mdomo nilipopiga kelele. Alafu yeye [Bi Kondoromoh] akaanza kunikata," Bi Allieu ameiambia BBC.

"Nilihisi aliponikata uuke wangu, aliingiza vidole ndani na kuvuta kitu alafu akakikata. walinizuia kichwa chini wakaendelea kunikata. Nilivuja damu sana. Nilijaribu kupiga kelele lakini walikuwa wamshindilia kitambara mdomoni mwangu," aliongeza.

Bi Kondoromoh amekana mashtaka lakini amekiri kumkeketa.

Amesema Bi Allieu alikutana naye nyumbani kwao akisema kuwa anazomewa na wanawake wenzake kwasababu hajakeketwa.

Image caption Ukeketaji ni utamaduni unaojaribu kusitishwa Afrika

Bi Kondoromoh ameongeza kuwa alimhudumia Bi Allieu baada ya kumkeketa.

Mwandishi wa BBC anasema polisi walimuokoa Bi Allieu siku kadhaa baada ya yeye kufanikiwa kuwapigia simu, na wanasema walimpata akiwa ''amedhohofika''.

Huku kukiwana wasiwasi kuhusu usalama wa Bi Allieu baada ya kundi la wakeketaji hao kufika hospitalini na vijiti kutaka wakabidhiwe, wanahrakati sasa wanataka ahamishwe kutoka Sierra Leone.

Inspekta Tarawallie ameiambia BBC kuwa uchunguzi unaendelea.

Ametetea uamuzi wa kumuachia Bi Kondoromoh akisema wakeketaji ''wamewazunguka''.