Trump 'aghadhabishwa na mauji ya mmarekani mweusi', Oklahoma

Donald Trump Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Republican Donald Trump

Donald Trump ameelezea wasiwasi wake kuhusu tukio la hivi majuzi ambapo polisi mmoja mweupe alimfyatulia risasi na kumuua mwanamme mmoja mweusi ambae hakuwa na silaha yoyote huko eneo la Tulsa, Oklahoma Marekani.

Akizungumza alipokuwa miongoni mwa kundi la makasisi wamarekani weusi kwenye kanisa moja katika jimbo la Ohio, mgombea huyo wa urais kutoka chama cha Republican ameelezea hisia zake kuwa tukio hilo limemsikitisha sana.

Terence Crutcher, mwenye umri wa miaka 40, alipigwa risasi siku ya Ijumaa na polizi huyo mzungu alipokuwa amesimama kando ya gari lake lililokuwa limeharibika.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mgombea wa kiti cha urais Marekani kwa tikiti ya Democratics Bi Hilarry Clinton.

Mgombea wa kiti hicho cha urais wa Marekani kwa chama cha Democratic Bi Hillary Clinton amesema " Ni sharti tabia hiyo ikome kabisa."

Swala hilo la polisi kuwaonea raia wamarekani weusi nchini humo, ni mojawapo ya mambo anayoyatilia maanani sana katika kampeni zake.

Lakini kwa upande wake Trump amejinadi kama ndio atakaeweza kuhakikisha sheria na utaratibu unaostahili unafuata kikamilifu, hivyo kuifanya kauli yake hii ya sasa, japo nadra, kuwa ya kutiliwa maanani zaidi katika kukashifu vitendo vya dhulma vinavyoendelezwa na polisi weupe dhidi ya raia weusi wasio na hatia yoyote.