Watu 10 wauawa katika mapigano makali Kananga DRC

Ramani

Ghasia za siku mbili katika mji wa Jamhuri ya kidemorasi ya Congo zimesababisha vifo vya watu 10.

Vikosi vya usalama Kananga vimekabiliana na wapiganaji wanaotaka kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi wao aliyeuawa na jeshi mwezi Agosti, maafisa na vyombo vya habari vinasema.

Wanamgambo hao waliushambulia uwanja wa ndege wa mji huo Ijumaa na kumuua mfanyakazi mmoja wa ndege, walioshuhudia wanasema.

Congo imekabiliwa na ghasia za miaka kadhaa na ukosefu wa utulivu kisiasa.

Maandaamano dhidi ya rais Joseph Kabila katika mji mkuu Kinshasa mapema wiki hii yamesababisha vifo vya watu 50, Umoja wa mataifa unasema.

Ripoti zinaarifu kuwa wapiganaji wanaomtii kiongozi wa kikabila aliyeuawa, Kamwina Nsapu, waliingia katika mji wa Kananga Alhamisi asubuhi.

Kituo cha Redio Okapi kinasema wanamgabo hao wamepambana na vikosi vya usalama na hatimaye walitimuliwa.

Walirudi Ijumaa na kukivamia kituo hicho cha ndege.

"Kulikuwa na mapigano makali yaliohusisha silaha ndogo na kubwa," anasema Killy Ilunga, aliyeuona mwili wa mfanyakazi wa ndege baada ya kuuawa.

"Waliingia katika ukumbi wa uwanja wa ndege. Mmoja wao alimpiga kwa rungu."

Idadi ya waliouawa haijathibitishwa, lakini ripoti zinasema idadi huenda ikawa kati ya watu 10 na 13.

Msemaji wa serikali Lambert Mende anasema hali imedhibitiwa.

Kuhusu BBC