Mkataba wa amani wa kihistoria watiwa saini Colombia

Santos na Timochenko Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Colombia Santos, kushoto na kiongozi wa waasi ajulikanaye kama Timochenko wamepeana mikono baada ya kutia saini mkataba huo

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos na kiongozi wa kundi la waasi wa FARC wametia saini mkataba wa amani kumaliza miongo mitano ya uhasama wa kivita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Katika hafla iliyofanyika huko mjini Cartagena wametumia kalamu iliyotengenezwa na risasi kusaini mkataba huo, na kisha kwa mara ya kwanza wakapeana mikono wakiwa ardhi ya Colombia.

Kiongozi wa kundi hilo la FARC kamanda Rodrigo Londono, anayejulikana vyema kwa jina Timochenko, amewaomba msamaha waathiriwa wote wa vita hivyo.

Waliohudhuria hafla hiyo walikuwa wamevalia mavazi ta rangi nyeupe, kuashiria amani.

Vita hivyo vilivyodumu kwa karibu miaka hamsini vilisababisha vifo vya watu 260,000 na wengine milioni sita kuachwa bila makao.

Rais Juan Manuel Santos amesema: "Colombia inasherehekea, ulimwengu unasherehekea kwa sasa kuna vita vimemalizika duniani."

Tutatimiza malengo yote, tutazidi nguvu changamoto zote na kugeuza nchi hii kuwa taifa ambalo tumekuwa tukitaka liwe, taifa la amani."

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Jamaa za watu waliouawa au kutekwa na waasi wa FARC wamehudhuria hafla hiyo Cartagena

Timochenko amesema Farc, kundi ambalo lilianza kama wanamgambo wa Chama cha Kikomunisti mwaka 1964, litaacha vita na kuingia katika siasa za amani.

"Tumezaliwa upya na kuzindia enzi mpya, kipindi cha maridhiano na kuendeleza amani," amesema.

"Sote tuwe tayari kuondoa 'silaha' kutoka kwenye nyoto zetu."