Mwezi wa Jupiter 'unatoa michirizi ya maji'

Europa
Maelezo ya picha,

Mwezi wa Europa ni moja ya maeneo ambayo wanasayansi wanatafuta iwapo kuna viumbe wanaoishi anga za juu

Wanasayansi wanasema wamepata ushahidi kuwa mojawapo ya miezi inayozunguka sayari ya Jupiter imekuwa ikimwaga maji mengi anga za juu.

Wanasayansi waliripoti mara ya kwanza kuhusu kuwepo kwa maji katika mwezi huo kwa jina Europa mwaka 2013 baada ya kuufuatilia kwa karibu kwa kutumia darubini kwa jina Hubble.

Sasa, wamethibitisha hilo baada ya kuitumia Hubble kuchunguza mwezi huo ulipokuwa unapita mbele ya sayari ya Jupiter (Mshtarii).

Walitumia darubini hiyo kuchunguza nguvu za mionzi ya jua kuona ikiwa ilikuwa inamezwa na kitu chochote kutoka kwa mwezi huo.

Walichunguza mara kumi, na mara tatu wakafuailia kilichoonekana kama "vidole vyeusi' vilivyokuwa vikitoka kwa Europa.

Mtaalamu aliyeongoza uchunguzi huo William Sparks, anasema hawezi kufikiria kitu kingine kinachoweza kusababisha jambo kama hilo kando na maji.

Michirizi hiyo ya inayoaminika kuwa ni ya maji ilionekana eneo ambalo miaka kadha iliyopita, wanasayansi waliokuwa wakitumia Hubble, waligundua oksijeni na haidrojeni, viungo vinavyounda maji.

Ni hatua muhimu kwa sababu Europa, sehemu yake kubwa imefunikwa na bahari ya maji, na ni moja ya maeneo ambayo inaaminika huenda kukawa na viumbe wanaoishi anga za juu kando na dunia.

Wanasayansi wanakadiria kwamba huenda wakaweza kuchota maji hayo na kuyafanyia uchunguzi kwa kupitisha chombo cha anga za juu kwenye michirizi hiyo.

Njia nyingine, ambayo inausisha kupeleka chombo ambacho kitatua katika mwezi huo na kuchimba kilomita nyingi ndani ya barafu ili kufikia maji, huenda ikawa na changamoto nyingi sana.

Maelezo ya picha,

Michirizi ya maji ambayo ilionekana katika mwezi kwa jina Europa

Maelezo ya picha,

Michoro kwenye sehemu ya juu ya mwezi wa Europa, ambao umefunikwa pakubwa na barafu

Michirizi ya maji imewahi kuonekana katika mwezi wa Enceladus, mwezi wenye barafu wa sayari ya Saturn (Sarteni).

Chombo cha anga za juu cha Cassini kwa sasa kinazunguka sayari hiyo na tayari kimepitia katika michirizi hiyo kufanya uchunguzi.

Hata hivyo, vifaa vya chombo hicho havina uwezo wa kuchunguza uwepo wa viumbe hai.