Kenya na Libya zatajwa katika mdahalo Marekani

Kenya na Libya zilitajwa katika mdahalo kati ya Clinton na Trump
Image caption Kenya na Libya zilitajwa katika mdahalo kati ya Clinton na Trump

Kenya na Libya ni miongoni mwa mataifa yaliotajwa wakati wa mdahalo wa urais nchini Marekani kati ya mgombea wa chama cha Democrat Hillary Clinton na mpinzani wake Donald Trump wa Republican.

Trump ambaye ni mfanyibiashara mkubwa aliitaja Kenya ,akidai kwamba bi. Clinton alianza kampeni mbaya dhidi ya rais Obama kwa kusambaza uvumi kwamba hakuzaliwa Marekani.

Libya pia ilitajwa katika mjadala huo wakati wagombea hao waliposhutumiana kuhusu ni nani aliunga mkono kuondolewa kwa aliyekuwa rais wa taifa hilo Muammar Gaddafi.

Bi Clinton ,ambaye alikuwa waziri wa maswala ya kigeni wakati wa uvamizi huo wa vikosi vvya Nato vilivyompindua kanali Gadafi 2011, aliyakabili matamshi ya Trump kwamba uamuzi wake ulikuwa wa makosa na kusema kuwa mfanyibiashara huyo pia aliunga mkono kuondolewa kwa Gaddafi.

Bi Clinton pia alidai kwamba bwana Trump alifanya biashara na kiongozi huyo wa Libya.