Mtoto azaliwa kutoka kwa mbegu za watu watatu

Dkt John Zhang akiwa na mtoto huyo Haki miliki ya picha NEW HOPE FERTILITY CENTRE
Image caption Dkt John Zhang akiwa na mtoto huyo

Mtoto wa kwanza aliyetengezwa kwa kutumia mbinu ya uzazi wa mbegu za watu watatu amezaliwa, jarida la kisayansi la New Scientist limetangaza.

Mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miezi mitano ana chembe chembe za DNA kutoka kwa mamake, babake pamoja na jeni za mfadhili.

Madaktari wa Marekani walichukua hatua hiyo kuhakikisha kuwa mtoto huyo wa kiume atakuwa huru kutokana na hali ya jeni ambayo mamake kutoka Jordan anabeba katika jeni zake.

Wataalam wanasema kuwa hatua hiyo ni mwamko mpya wa kimatibabu na inaweza kusaidia familia nyingine zilizo na hali za jeni zisizokuwa za kawaida.

Lakini wameonya kuwa uchunguzi wa mara kwa mara wa mbinu hiyo mpya ya kiteknolojia inayoitwa ufadhili wa Mitochondrial unahitajika.

Mitochondria ni vyumba vidogo vidogo ndani ya kila seli ambavyo hubadili chakula kuwa nguvu inayotumika mwilini.

Baadhi ya wanawake hubeba jeni zilizo na kasoro na wanaweza kupitisha jeni hizo hadi kwa watoto wao.

Wanasayansi waliohusika katika shughuli hiyo walisafiri hadi Mexico kwa sababu huko hakuna sheria za kuzuia shughuli kama hiyo ya kimatibabu.

Walichukua sehemu muhimu za chembe za kinasaba (DNA) kutoka kwa yai la mama, na DNA ya mitochondria kutoka kwa yai la mfadhili na kuunda yai lenye afya ambalo lilitungshwa mbegu kutoka kwa baba.

Matokeo yake ni kuzaliwa kwa mtoto mwenye 0.1% ya DNA kutoka kwa mfadhili na jeni nyingine zote, zinazoamua sifa kaa vile rangi ya nywele na macho kutoka kwa mama na baba.

Image caption Teknolojia mpya ya uzazi ndio iliotumika kumtengeza mtoto huyo

Dkt John Zhang, mkurugenzi wa kimatibabu katika hospitali ya New Hope Fertility Centre jijini New York City, anasema yeye na wenzake walitumia njia hiyo kupata viinitete vitano, lakini wakastawisha kimoja tu.