Rais wa Ushelisheli James Michel ajiuzulu

James Michel
Image caption James Michel ameongoza kwa miaka 12

Rais wa taifa la Ushelisheli James Michel ametangaza kwamba atajiuzulu, siku chache baada ya chama chake kushindwa kwenye uchaguzi wa wabunge.

Kiongozi huyo wa umri wa miaka 72 amekuwa madarakani tangu 2004 na chama chake kimetawala taifa hilo la visiwa kwa miongo minne.

Alifanya tangazo hilo la ghafla kupitia runinga siku ya Jumanne ambapo aliahidi kuondoka madarakani ifikapo 16 Oktoba.

"Baada ya kuhudumu miaka 12 kama rais, wakati wangu kukabidhi madaraka kwa kiongozi mpya umewadia. Kiongozi mpya atafikisha Ushelisheli hatua hiyo nyingine ya ufanisi."

Aprili, bunge la nchi hiyo liliidhinisha marekebisho ya katiba na kupunguza muda wa rais kuongoza kuwa mihula miwili ya miaka mitano badala ya mihula mitatu ya miaka mitano.

Mrithi wake atakuwa makamu wa rais wa sasa Danny Faure, 54, ambaye amehudumu katika wadhifa huo tangu 2010.

Atalishwa kiapo 16 Oktoba na kuongoza kipindi kilichosalia cha muhula wa sasa wa Michel.

Muungano wa vyama vya upinzani wa Seychellois Democratic

Alliance ulishinda viti vingi kwenye uchaguzi uliofanyika 8-10 Septemba katika taifa hilo la visiwa 115.

Upinzani ulipata viti 15 nacho chama cha upinzani cha Parti Lepep kikashinda viti 10.

Upinzani umeahidi kufanya kazi na rais kwa maslahi ya taifa.

Parti Lepep kimekuwa madarakani tangu 1977, mwaka mmoja baada ya uhuru, na kimeshinda uchaguzi tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi 1993.

Michel alikuwa tayari amehudumu mihula miwili ya miaka mitano mitano na alikuwa ameanza kuhudumu muhula wa tatu Desemba mwaka jana.