Tetemeko: Magufuli awafuta kazi maafisa wakuu Kagera

Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa wakiwa na mfano wa hundi ya mchango kutoka kwa Balozi wa India Tanzania Sandeep Arya katika ikulu jijini Dar es Salaam. Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania
Image caption Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa wakiwa na mfano wa hundi ya mchango kutoka kwa Balozi wa India Tanzania Sandeep Arya katika ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Tanzania John Magufuli amewafuta kazi maafisa wawili wakuu wa serikali mkoani Kagera kutokana na tuhuma za kufungua akaunti iliyofanana na ile ya kukusanya pesa za kusaidia waathiriwa wa tetemeko la ardhi.

Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Bw. Steven Makonda.

Taarifa kutoka ikulu imesema kiongozi huyo amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa wamefungua akaunti nyingine kwa jina "Kamati Maafa Kagera" kwa lengo la kujipatia fedha.

Rais Magufuli ameagiza vyombo vya dola vichukue hatua dhidi ya wote waliohusika katika njama za kufungua akaunti hiyo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw. Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika katika njama hizo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Rais kupokea msaada wa Shilingi milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India Narendra Modi za kusaidia waathiriwa wa tetemeko hilo la ardhi lililotokea 10 Septemba, 2016.

Bw Majaliwa ametoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kuchangia misaada kwa ajili ya walioathirika kwa kutumia akaunti rasmi ya "Kamati Maafa Kagera".